Wagombea TFF kujulikana leo


OFISA HABARI WA TFF, ALFRED LUCAS.

KAMATI ya Uchaguzi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) leo inatarajiwa kutoa orodha ya majina ya wanachama waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Shirikisho hilo.

Wadau 74 walijitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha kwa kamati hiyo wakisubiri majina yatakayopitishwa.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema kuwa kamati hiyo yenye jukumu la kusimamia uchaguzi huo itatoa majina leo.

"Kamati inafanya kazi yake na mambo yakikamilika huwenda kesho (leo) wakatangaza majina ya wale waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kama walivyoomba," alisema Lucas.

Kamati hiyo ilianza kukaa na kupitia fomu za wagombea juzi katika hoteli moja ya jijini Dar es Salaam ambapo wanapitia fomu zote za wagombea wanaowania nafasi mbalimbali.

Wadau watano wamejitokeza kuwania nafasi ya Urais ambapo yumo Jamal Malinzi, Fredrick Mwakalebela, Omari Madega, Athuman Nyamlani pamoja na Wallace Karia.

Nafasi ya Umakamu Mwenyekiti wamejitokeza wadau wanne akiwemo Richard Selasela, Michael wambura, Geofrey Nyange 'Kaburu' pamoja na Mlamu Nghambi huku wadau 65 wakijitokeza kuwania nafasi ya ujumbe kupitia kanda 13 tofauti.