Emmanuel Okwi wa Simba
Simba wikiendi ijayo itacheza na Mtibwa mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, halafu itavaana na Njombe Mji Oktoba 21, kabla ya Oktoba 28, mwaka huu kucheza na Yanga katika ligi hiyo.
Okwi, raia wa Uganda, ndiye anayeongoza kwa ufungaji katika ligi hiyo akiwa na mabao sita akifuatiwa na Mohammed Rashid wa Prisons mwenye mabao manne. Pia Habib Haji wa Mbao FC na Shiza Kichuya wa Simba nao wana mabao matatu kila mmoja.
“Najua Yanga ni timu kubwa na ndiyo mabingwa watetezi wa ligi kuu, ila ukiangalia msimamo wa ligi kuu ulivyo kwa sasa nalazimika zaidi kuitazama Mtibwa ambayo ndiyo tutacheza nayo kabla ya Yanga.
“Mtibwa imekuwa na matokeo mazuri, hivyo nina kila sababu ya kuiwazia hiyo na baada ya mchezo huo na matokeo yake ndiyo yatanifanya kuifikiria tena Yanga jinsi gani tutapambana nayo,” alisema Okwi.
Okwi alisema anachokifanya kwa sasa ni kuendelea kufunga mabao bila ya kujali kama atakuwa mfungaji bora au la bali anachoangalia kwanza ni kuipa ushindi timu yake, mengine yatafuata.
Simba ndiyo inayoongoza katika msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 11 sawa na Mtibwa na Azam FC, huku Yanga ikishika nafasi ya sita ikiwa na pointi tisa. Zote hizo zimecheza mechi tano mpaka sasa.