Dk Shika apokewa ‘kifalme’ Shinyanga

Kahama. Dk Louis Shika ‘bilionea’ aliyejizolea umaarufu baada ya kuibuka katika mnada wa kununua nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi ametua mjini Kahama na kupokewa na watu wengi.

Mapokezi ya Dk Shika aliyetua mjini hapa kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Chuo cha Afya cha Kahama (Kahama College of Health Science), yameongozwa na msururu wa magari zaidi ya 50 na kupita kwenye mitaa mbalimbali kabla ya kuelekea chuoni, Kata ya Mwendakulima, nje kidogo ya mji wa Kahama.

Mapokezi hayo leo Alhamisi Novemba 23,2017 yameongozwa na Mkurugenzi wa chuo hicho, Yona Bakungile kuanzia uwanja wa ndege wa Buzwagi.

Ili kupata fursa ya kusalimiana na kuwapungia mikono mamia ya watu waliojipanga barabarani kumshuhudia baada ya kupata habari zake, Dk Shika alipanda gari la wazi, jambo lililofanya hata baadhi ya watu wenye shughuli zao maeneo alikopita kuzitelekeza kwa muda kwenda kumshuhudia.

Mwenyeji wake alonga
Akizungumza na Mwananchi sababu za kuamua kumwalika Dk Shika katika mahafali ya chuo chake, Bakungile amesema ni kutokana na utaalamu wake wa masuala ya tiba ya binadamu na umaarufu wake unaoendelea kuvuma nchini.

“Chuo changu kinatoa mafunzo ya afya ya binadamu; licha ya umaarufu wake nchini kwa sasa, Dk Shika ni miongoni mwa wataalamu katika fani ya utabibu ndiyo maana nimemwalika. Naamini atawashauri na kuwapa hamasa wahitimu na wanafunzi wanaoendelea,” amesema Bakungile

Dk Shika atangaza neema ya ada
Akihutubia mbele ya umati uliojitokeza, wakiwemo wananchi waliofuata msafara wake kutoka mjini umbali wa zaidi ya kilomita tatu kutoka chuoni, Dk Shika ameahidi kulipa ada na gharama za masomo kwa wanafunzi ambao wana uwezo kimasomo lakini wazazi au walezi wao hawawezi kuwalipia.

“Natambua umuhimu wa masomo ya afya na ughali wa malipo yake kwa Watanzania wenye kipato cha chini; nitawalipia wanafunzi wote wenye uwezo darasani lakini wazazi au walezi wao hawawezi kugharamia masomo yao,” ameahidi Dk Shika.

Amesema uamuzi wake unalenga kuhakikisha Taifa linakuwa na wataalamu waliobobea katika taaluma ya utabibu.

Mkurugenzi wa kituo cha huduma ya mawasiliano ya mtandao cha Mary Internet, Mary Patrick ambaye ni kati ya walioshangazwa na ujio na msafara wa magari ametaka Dk Shika kutumia vyema umaarufu wake kusaidia jamii.

Mwananchi: