F Balozi Seif: Wakati Umefika Kutowapa Nafasi Za Uongozi Wanaohama Chama | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Balozi Seif: Wakati Umefika Kutowapa Nafasi Za Uongozi Wanaohama Chama

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amesema wakati umefika kwa Wananchama wa Chama cha Mapinduzi kutowapa nafasi za Uongozi wanachama wenye tabia ya kuhama Jimbo moja na kuhamia Jimbo jengine.

Alisema Wanachama hao hufikia uamuzi wa kuyakimbia Majimbo yao ya zamani na kutaka kuhamia majimbo mapya baada ya kujibaini kutowatumikia vyema Wanachama na Wananchi wao katika kipindi walichoomba ridhaa ya kuwawakilisha katika nafasi za Ubunge na Uwakilishi kwenye vipindi vya awali.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Magharibi wa kuwachagua Viongozi watakaouongoza Mkoa huo kwa kusaidiana na viongozi wengine katika kipindi cha Miaka Mitano ijayo 2017 – 2022 ambao ulifanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema uzoefu umebainisha wazi kwamba Wawakilishi na Wabunge wanaoendelea na majukumu yao ndani ya Majimbo yao hukumbwa na matatizo ukiwemo ushawishi, fitna na majungu yanayobuniwa na wale wanaotaka nafasi hizo jambo ambalo huchangia kukosekana kwa uwajibikaji.