KAMA kuna wakati mgumu au tunaofanya maamuzi bila umakini ni huu wa kuchagua mchumba. Kumbuka kwamba lengo la kuchagua mchumba ni kupata mwenzi wako wa maisha. Tofautisha kuwa na mchumba na kuwa na mpenzi.
Kuna hatua za kupitia kufikia katika jambo hili; kwanza urafiki, pili mapenzi, tatu uchumba na mwisho ndoa. Hawezi kuwa mchumba kama hakuwahi kuwa mpenzi wako na hawezi kuwa mpenzi wako kama hakuwahi kuwa rafiki yako, hivyo basi haya mawili ya kwanza hukufanya wewe kijana kupata mchumba.
Baada ya kuwa wapenzi, mkashibana na kila mmoja akakubaliana na mwenzake, ndipo hatua hii muhimu huchukuliwa yaani mwanaume kutuma mshenga kwa wazazi wa mwanamke na uomba kuchumbia. Mchumba lazima achumbiwe, kama hujamchumbia huyo bado ni mpenzi tu. Kuchumbia maana yake ni kutoa posa na wazazi wa mwanamke kukuridhia kuwa wewe ndiwe haswa utakuwa mume wa binti yao.
Katika makala hii ya mahusiano leo, nataka kukujuza hatua kumi muhimu sana unapotaka kuchagua mchumba, nikiwa na maana kuwa hatua hizi zitaanzia kwenye urafiki, upenzi na mpaka utaingia katika uchumba na Mungu akipenda mtaingia katika ndoa. Siku hizi kuna msemo wanasema kuwa ‘kosea yote lakini si kuchagua mke’. Wanaosema maneno haya wapo sahihi kabisa, na ninawaunga mkono, hakika usifanye makosa kwenye hili.
Yote kwa yote tukumbuke kuwa hakuna binadamu aliye kamili, hivyo huwezi kupata mchumba malaika, lakini katua hizi ni kwamba utapata mchumba mzuri na zitakusaidia kupunguza matatizo ambayo yangekukabili kama ungekurupuka.
KWANZA- Ni ya mwanamke/mwanaume mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi anayemhitaji katika maisha yako. Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake na kila mwanamke anaye wake wa maisha pia. Hivyo asiyekufaa wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe kujitambua kwanza ili umtambue umtakaye.
Wanawake/wanaume wengi hawafahamu wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua nini. Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi, wakachezewa na kuumizwa moyo bure.
PILI- Ni kuketi chini na kuorodhesha vigezo stahili vya mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, ana upungufu wake.
TATU- Anza kumsaka kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako hutambulika kwa moyo kurithika na mwili kusisimka.
NNE – Kuanzisha safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.
Katika uchunguzi huu mwanamke/mwanaume unayetafuta mpenzi huna budi kupitia na kumlinganisha huyo uliyempata na vigezo ulivyojiwekea. Zoezi hili liendane na kuweka alama ya tiki kila anapobaini kuwa mwanaume/mwanamke unayemchunguza umepata moja ya vigezo vyako. Lakini pia uweke alama ya kosa kwa kila kasoro unayoivumilia na ile usiyoivumilia.
TANO – Ujipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza huyo mwanaume/mwanamke, kisha uketi chini na uanze kujumlisha alama za vigezo ulivyovijiwekea na jinsi mtu huyo alivyopata au kukosa.
Ikibainika mwanaume/mwanamke uliyemchagua amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo vilivyowekwa, basi ujue kuwa anafaa. Kuhusu alama chache alizikosa anaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati wa maisha ya ndoa.
Lakini angalizo kubwa kabisa ni kwamba mwanaume/mwanamke akionekana kuanguka katika kasoro zisizoweza kuvumilia kwa zaidi ya alama tatu. Yaani kwa mfano ni mlevi, mwizi, muongo, mbishi na katika hizo kashindwa 3, huyu hafai, ni vema akawekwa kando kwani huwezi kubeba kero 3 kwa pamoja katika maisha.
SITA – Kusajili mapenzi yenye malengo yanayotekelezeka. Lazima baada ya kuchunguzana kwa kina wapenzi watengeneze muongozo wa mapenzi yao. Wasiwe kama wanyama, lazima mipango ya wapi wametoka walipo na wanapokwenda.
Hata hivyo watalaam wanasema lazima wapenzi wapime umakini wao kwa vitendo. Kama wamekubaliana kuoana, suala la mume kwenda kujitambulisha kwa wakwe na hatua ya kuiendea ndoa ionekane. Usiri usiwepo tena. Kila mmoja amuone mwenzake kama sehemu ya maisha yake na mara zote wasaidiane kwa ukaribu.
SABA – Ni vema ndugu wakashirikishwa ili kuwapa nafasi na wao ya kuamua kama mapenzi hayo ni budi yakaendelea au yakasitishwa. Ni ukweli ulio wazi kwamba licha ya wengi kupuuza maamuzi ya ndugu kwa madai ya kuwa hawana nafasi kwa wapenzi wao, lakini uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi wengi huacha kutokana na sumu za ndugu hasa pale wanapokuwa wameonesha kutounga mkono uhusiano wa wanaotaka kuoana
NANE – Hatua hii ni ya kuweza kuzungumzia ufanyaji mapenzi, hapa nina maana kama wapenzi wamejizuia kwa muda mrefu na wanahisi kuchoka wanaweza kujadiliana kuhusu hilo na kuamua ufanyaji huo wa mapenzi una lengo gani, kama ni kuburudisha miili basi suala la afya na uzazi salama litazamwe. Katika hili lazima sheria za dini zizingatiwe, kwani kwa kufanya ngono kabla ya ndoa ni kwenda kinyume na usafi wa moyo. Wengine husema ‘lazima kujaribu kuona kama uzazi upo’, katika hili lazima kuwa makini, utafiti wa ukamilifu katika uzazi unaweza kuchunguzwa kitaalamu bila kuhusisha tendo la ngono. Hivyo wapenzi watembelee vituo vya afya na kuweza kufanya vipimo vya yote haya.
TISA – Kutimizwa kwa ahadi ya kuoana ni hatua ya tisa ambayo nayo si busara ikachukua muda mwingi kutekelezeka, kwani ucheleweshaji mwingi wa ndoa nao huvunja moyo na mara nyingine umewafanya wengi kutoaminiana.
KUMI – Kuamua kuwa mwili mmoja kwa kuvumilia na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zote za maisha ukiwemo mkwamo na dhiki ambazo huchangia sana ndoa nyingi kuvunjika. Hapa pia ni wajibu wa wanandoa kuchukuliana udhaifu na kusaidia, kuwa tayari kujifunza na kujali zaidi upendo kuliko hisia za mwili ambazo wakati mwingine hudanganya na hivyo kumfanya mwanandoa asivutiwe na mwenzake.
Mwisho ni kwamba kanuni hizi huwafaa watu wazima mapenzi ya kitoto hayawezi kujenga misingi hii imara mara nyingi ni kudanganyana, kuharibiana maisha, kupeana mimba na maradhi. Utulivu na usikivu ni jambo muhimu sana katika hatua hii. Kumbuka ndoa ni kifungo cha ukamilifu katika upendo wa kuwa kitu kimoja.