Maandamano yaua mtu mmoja na kujeruhi watano

Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 55 amekufa baada ya maandamano ya kupinga hatua kali za kiuchumi za serikali, shirika la habari la serikali la Tunis Afrique Presse (TAP) limeripoti.

Kwa mujibu wa TAP, watu wengine watano walijeruhiwa katika maandamano hayo yaliyofanyika katika mji wa Tebourba ulioko kilomita 40 magharibi mwa jiji la Tunis.

Waziri wa Mambo ya Ndani alithibitisha Jumatatu jioni kwamba mtu mmoja anayesadikiwa kuwa na umri wa miaka 55 alifariki baada ya kufikishwa hospitalini akiwa na dalili za kizunguzungu.

Hata hivyo mitandao ya kijamii Jumatatu ilieleza kwamba mtu huyo alikufa baada ya kugongwa na gari la vikosi vya usalama jambo ambalo serikali inakanusha ikisema huenda alivuta gesi ya kutoa machozi na ikamsababishia matatizo katika mfumo wa upumuaji.

Maandamano mengine yalifanyika katika maeneo kadhaa nchini Jumatatu baada ya serikali kutangaza ongezeko la kodi katika Sheria ya Fedha yam waka 2018.

Bajeti ya Serikali iliyoanza rasmi kutekelezwa Januari Mosi, ilipandisha bei ya mafuta na ikaanzisha kodi mbalimbali zinazohusiana na vifaa vya ujenzi.

Katika jiji la Sidi Bouzid katikati ya Tunisia, waandamanaji walijimwaga mitaani kwa siku ya pili mfululizo Jumatatu kupinga ongezeko la bei na wakatoa wito kupitiwa upya Sheria ya Fedha, liliandika TAP likidokeza maandamano zaidi yanatarajiwa siku za baadaye.

Miongoni mwa sababu ya maandamano hayo ni mfumko wa bei ambao umesababisha kuongezeka kwa kodi katika bidhaa zinaingizwa nchini kama magari na bidhaa nyingine.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items