Makao Mkuu yazindua mpango mkakati wa kupambana na Ukimwi


MKOA wa Dodoma amezindua mpango mkakati wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi unaozingatia uhamiaji wa watu ambao wanazifuata fursa zinazotokana na makao makuu ya serikali kuhamia Dodoma.

Mkuu wa Mkoa Dk. Binilith Mahenge,akizungumza katika uzinduzi huo, alisema wadau wa mkoa wa Dodoma wana jukumu la kuutafsiri mpango mkakati huo kwenye mazingira yao ili kuutumia kupanga mipango ya kudhibiti maradhi hayo.

Alisema mpango huo umezingatia ongezeko la watu wanaofuata fursa za ujio wa serikali mkoani humo na kwamba usalama wa maisha na kuwa na Dodoma isiyo na Ukimwi unawezekana.

Alizitaka mamlaka zote zinazohusika na wadau mbalimbali zingatieni vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango Mkakati ili kufikia lengo la kidunia na kitaifa la kuhakikisha angalu asilimia 90 ya watu wenye Virusi vya Ukimwi(VVU) wanajua hali zao.

“Pia asilimia 90 ya watu waliojua hali zao waanze kutumia dawa na kati yao asilimia 90 wawe wamefubaza virusi hivyo kupunguza uwezo wa kuambukiza (90-90-90) ifikapo 2020,”alisema.

Dk. Mahenge alisema mamlaka zizingatie vipaumbele kuhakikisha 2030 maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na  Ukimwi vinakuwa sifuri (0-0-0).

“Kila Wizara na Idara zinatakiwa zihakikishe zinaandaa Sera ya Ukimwi mahala pa kazi na kuwapa stahiki zao watumishi wanaoishi na VVU,”alisema Mkuu huyo

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa, Rehema Madenge, alisema mchakato wa kuandaa Mpango Mkakati mpya kwa mkoa huo ulichagizwa na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma.

Alisema mkakati huo wa miaka mitatu 2017/2018 - 2020/2021 ni shirikishi na umehusisha wadau mbalimbali kwenye ngazi zote muhimu na utekelezaji wake pia utakuwa shirikishi.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS),  Richard Ngirwa, alisema ripoti ya utafiti wa Matokeo ya Viashiria vya VVU na Ukimwi uliofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo (2016/17) imethibitika kuwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo nchini ni asilimia 4.8 kwa wanawake na wanaume wa umri wa miaka 15-49.

Alisema kila mtu ana wajibu na mchango mkubwa katika mapambano na ugonjwa huo na kuiomba jamii isiiachie serikali peke yake.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items