Watu wanne mbaroni kwa kumiliki Vichwa vinne na Nyara za Serikali


WATU wanne wanashikiliwa na polisi mkoani Manyara kwa kukutwa na nyara za serikali, wakiwa na vichwa vinne vya wanyamapori waliowawinda na kuwaua.

Aidha mtu mmoja anashikiliwa na jeshi hilo kwa kupatikana na dawa za kulevya.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Augustino Senga, alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Kamanda Senga alisema watu hao walikamatwa majira ya saa 4:30 usiku wa Januari 22, mwaka huu katika kijiji cha Kimana wilayani Kiteto.

Alisema askari waliokuwa doria waliwatia mbaroni  watuhumiwa hao ambao aliwataja kuwa ni Piason  Ramadhan (68), mkulima  mkazi wa Orkeni, Ramadhani Mohamed (26), mkulima mkazi wa Songe, Rashid Ramadhani (17) mkulima mkazi wa Orkine na Abuu Athumani (14) mkulima na mkazi wa Orkine.

“Askari polisi wakiwa na Kikosi cha Kuzuia Ujangili waliwakamata watu wanne wakiwa na vichwa vinne vya wanyama waliowawinda na kuwaua, silaha mbili aina ya gobore na nyama pori.

Aidha, Kamanda Senga alisema magobore waliyokutwa nayo moja lilikuwa na namba Hd 831 na jingine  lisilo na namba, yote yakiwa yametengenezwa kienyeji.

Alisema watuhumiwa walikutwa pia na unga wa baruti, maganda 20 ya risasi za bunduki aina shortgun, vifaa mbalimbali vya kutengenezea risasi za kienyeji na nyaya nne za kutegea wanyama.

Katika hatua nyingine, alisema jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kupatikana na dawa ya kulevya aina ya heroine.

Alisea tukio hilo lilitokea Januari 23, majira ya saa 4:30 usiku katika kijiji cha Songambele kata ya Mirerani wilayani Simanjiro.

Alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Shaban Nassoro (40) mkulima mkazi wa Songambele.Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na kete 75 za heroine.

Kamanda Senga alitumia fursa hiyo kuwaonya watu wanaojihusisha na uhalifu kuacha mara moja na kutafuta kazi nyingine za kufanya kwa kuwa wakipita  mkoani mwake hawatakuwa salama.

“Wasifikiri mkoa huu ni kisiwa cha kupitisha dawa za kulevya na kufanyia ujambazi, hapana," alisema Kamanda Senga. "Tutawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.”

Alisema Polisi itaendelea kufanya misako na doria  za mara kwa mara ili kuwabaini wahalifu.

Aidha alisema wataendelea kuzitumia kamati mbalimbali za ulinzi na usalama kuanzia ngazi za chini ili ziwasaidie kupambana na uhalifu.

Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano na jeshi hilo kuwabaini wahalifu ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items