MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura), imetangaza kupanda kwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na mamlaka hiyo, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yaliyoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, zimeongezeka ikilinganishwa mwezi uliopita.
Bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote yaliyoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam ziliongezeka pia mwezi uliopita kulinganisha na bei zilizotangazwa Disemba 6, mwaka jana.
Kwa Januari, bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa ziliongezeka kwa Sh. nane kwa lita (petroli), Sh. 34 kwa lita (dizeli) na Sh. 89 kwa lita (mafuta ya taa)
Taarifa hiyo ambayo ilisainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany, ilieleza kuwa bei hizo mpya zilianza kutumika jana.
"Pamoja na kutambua bei kikomo za bidhaa mbalimbali za petroli nchi nzima ni muhimu kuzingatia bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote yaliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam kuwa zimeongezeka ikilinganishwa na toleo la Januari 3, mwaka huu," ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema bei ya rejareja kwa petroli imeongezeka kwa Sh. 59 kwa lita ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 2.70.
"Dizeli imeongezeka kwa Sh. 46 kwa lita ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 2.30 na mafuta ya taa imeongezeka kwa Sh. 24 kwa lita ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 1.17 sawia," ilisema.
Taarifa hiyo ilisema kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli ilikuwa ni Sh. 58.57 kwa lita sawa na asilimia 2.85, dizeli Sh. 46.48 sawa na asilimia 2.44 na mafuta ya taa Sh. 23.75 sawa na Sh. 1.24.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya rejareja ya petroli kwa mkoa wa Dar es Salaam kwa lita ni Sh. 2,226, dizeli Sh. 2,065 na mafuta ya taa ni Sh. 2,055.
Aidha, taarifa hiyo ilitaja bei ya rejareja ya petroli kwa lita kwa mkoa wa Arusha ni Sh. 2,278, dizeli Sh. 2,163 na mafuta ya taa ni Sh. 1,995.
Kwa mkoa wa Dodoma taarifa hiyo ilitaja bei ya rejareja ya mafuta ya petroli kwa lita kuwa ni Sh. 2,285, dizeli Sh. 2,123 na mafuta ya taa ni Sh. 2,113.
Taarifa hiyo ilisema bei za mafuta katika soko la dunia kwa mwezi Novemba mwaka jana ziko juu kwa zaidi ya asilimia sita ikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba, 2017.
