Utetezi kwa wenye Ualbino wapatikana


SHIRIKA la Kimataifa la kutetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), pamoja na Mtandao wa dini mbalimbali kwa watoto (GNRC), wameanzisha mradi wenye lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino nchini.

Mradi huo uitwao ‘Haki yetu’ utatekelezwa katika mikoa yenye vitendo vingi vya mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo ni Geita, Kigoma, Shinyanga, Simiyu na Mwanza kwa mwaka mmoja.

Ofisa uraghibishaji wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Watu wenye Ualbino (UTSS), Kondo Seif, aliyasema hayo wakati wa warsha ya kuwaelimisha viongozi wa dini nchini kuhusu mradi huo.

“Lengo la mradi huu ni kuwaelimisha wananchi kuhusu ualbino, na leo tumekutana na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali ambao wataenda kuwaelimisha waumini wao katika siku za ibada,” alisema Seif.

Aliongeza Tanzania ni nchi ya amani, hivyo kila Mtanzania ana haki ya kuishi huru, na watu wenye ulemevu wa ngozi hawapaswi kuishi kwa hofu wala katika makambi.

Naye Mratibu mkazi wa GNRC, Yusuph Masanja, alisema viongozi wa dini ni watu muhimu katika kuwaelimisha waumini wao kuhusu watu wenye ualbino na ndiyo sababu wanapewa elimu ya ualbino.

“Tunaamini kupitia dini Tanzania inaweza kubadilika, watu wenye ualbino wanaishi kwa hofu nchini, na tatizo la ukatili dhidi ya watu wenye ualbino bado lipo nchini, elimu bado haijawafikia wananchi,” alisema Masanja.

Amiri Mkuu wa baraza kuu na Taasisi za kiislamu, Sheikh Mussa Yusuph Kundecha, alisema  ualbino ni suala la kibinadamu na lipo duniani kote.

Alisema sababu kubwa ya Tanzania na nchi nyingi za Afrika matukio ya vitendo vya ukatili kuendelea ni kwa sababu hakuna sheria madhubuti zinazosimamiwa kupambana na vitendo hivyo.

“Serikali inapaswa kuweka na kusimamia sheria dhidi ya watu watakaokamatwa wakijihusisha a vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. Kwa nini nchi za ulaya vitendo hivi hakuna? Kwa sababu sheria zao ni kali,” alisema Sheikh Kundecha.

Alisema Tanzania hakuna sheria kali zilizowekwa kuhusu watu watakaohusika katika kuwafanyia vitendo vya ukatili watu wenye ulemavu wa ngozi. 
Mpya zaidi Nzee zaidi