“Ni kosa polisi kujichunguza kwa Matukio yanayowahusu”: Asasi za Kiraia

Asasi za Kiraia nchini zimetaka iundwe Tume huru ya uchunguzi wa kifo cha Mwanafunzi wa NIT, Akwilina Akwiline itakayoundwa na Taasisi za Dini, Vyombo vya Habari, Majaji, Mahakimu, Polisi na Baraza la Vyama vya Siasa.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Equality for Growth, Jane Magigita amesema kuwa Asasi za kiraia zimesikitishwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Tunapendekeza iundwe Tume huru ya uchunguzi itakayohusisha Azaki, Taasisi za dini, vyombo vya Habari, Baraza la vyama vya siasa, wanahabari, Majaji, Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora kufanya uchunguzi juu ya vifo na vitendo vya utekwaji na utesaji,”-Magigita

“Pia ni kosa kubwa kuwaachia Polisi kujichunguza wenyewe katika matukio yanayowahusu,” -Magigita

Mbali na hilo, pia ameiomba Serikali itazame upya suala la upatikanaji wa Katiba mpya na mchakato wake uanze mwaka huu kwani ndiyo suluhisho la matatizo mbalimbali yanayotokea katika Jamii kwa sasa.