Tanzania yakabiliwa na uhaba wa wahandisi wa kike

Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa wahandisi wa kike jambo ambalo linasababisha, kukwamisha maendeleo katika sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini, Patrick Barozi katika semina ya wahandisi kanda ya Kaskazini inayofanyika jijini Arusha.

Lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo wahandisi wa kike kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Arusha Tanga, Kilimanjaro na Manyara Barozi ameeleza kuwa sekta ya uhandisi imekuwa haina wataalamu wa kike kutokana na wanafunzi wa kike kutoyapa kipaumbele masomo ya sayansi jambo linalofanya kuwepo kwa changamoto hiyo

Alisema kuwa hadi sasa kuna asilimia 10 tu ya wahandisi wa kike kulinganisha na wahandisi wa kiume ambao idadi yao ni asilimia 90.

Msajili huyo alisema kuwa nchi ya Tanzania imekuwa ikikuza ustawi wa utoaji wa wanafunzi wengi zaidi ya asilimia 60 kulinganisha na nchi za Kenya na Rwanda.

Alisema nchi hizo ustawi wao ni mdogo ukilinganisha na Tanzania kwani wahandisi wa kanda ya Kaskazini ni 491 na huku waliosajiliwa ni 219 pekee.

Kutokana na changamoto hizo, alieleza kuwa sera ya serikali ya awamu ya tano ya viwanda ina uhitaji mkubwa sana wa wahandisi ili taifa kufikia malengo na hivi sasa wameanzisha kampeni ya kuhamasisha wanafunzi waliyopo mashuleni kusoma masomo ya sayansi.

Awali, akifungua semina hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Uendelezaji wahandisi kitaaluma hapa nchini PDAC , Profesa Esnat Chaggu alisema licha ya wahandisi kuwa na manufaa makubwa katika taifa aliwataka kutumia fursa za changamoto zilizopo ili kufanikisha miradi mbalimbali na kufikia malengo tarajiwa katika tasnia ya uhandisi na taifa kwa ujumla.