Hivi ndivyo Belle 9 alivyompa jina Agness Masogange


Abednego Damian ‘Belle 9′

MKALI wa Bongo Fleva, Abednego Damian ‘Belle 9′ ndiye ‘aliyembatiza’ jina la Masogange mrembo maarufu wa kuuza sura kwenye video za wasanii, marehemu Agness Gerald.

Kabla hawajakutana na kumuuzisha sura kwa mara ya kwanza katika wimbo wake wa Masogange, wengi walikuwa hawamfahamu Masogange, lakini baada ya wimbo huo, kila mmoja aliweza kumjua kutokana na kuutendea haki wimbo huo.

Mbali na kuuza sura, Masogange alikuwa na sifa ya ziada iliyowafanya wasanii wengi wavutiwe kufanya naye kazi. Muonekano wake ulikuwa kivutio kikubwa na hapo ndipo umaarufu wake ulipozidi kushika kasi kama moto wa kifuu.

Katika makala haya, tumezungumza na Belle 9 ambaye amefunguka mambo mengi kuanzia walipokutana, hadi kufanya video yake ya Masogange na jinsi alivyoguswa na kifo chake kilichotokea Aprili 20, mwaka huu katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar:


Over The Weekend: Mambo vipi Belle na pole sana kwa msiba.

Belle: Nashukuru sana, ndiyo hivyo kazi ya Mungu haina makosa.

Over The Weekend: Watanzania wangependa kujua labda ilikuwaje hadi ukakutana na Masogange na kufanya naye kazi.

Belle: Iko hivi, mimi nilikuwa nimesharekodi ule wimbo (Masogange) na nilikuwa nimeshautoa kwa hiyo nilikuwa kwenye hatua ya kurekodi video. Nilikuwa karibu sana na AY ambaye alinikutanisha na DJ wake anaitwa Asa huyo Asa ndiye aliyenikutanisha na Agness tulikuwa tunaenda kwake maeneo ya Sinza kwa ajili ya kuandaa video hiyo ndipo Asa akapendekeza tumtumie mrembo huyo.

Over The Weekend: Ina maana wewe ulikuwa hujawahi kabisa kumuona Masogange? Ulimuaminije kufanya naye kazi?

Belle: Kwa kweli sikuwa nikimfahamu kabla, lakini kwa kuwa nilikutanishwa na mdau ambaye ni DJ wa AY, niliamini kwamba hawawezi kuniangusha na kweli akafanya maajabu katika video.

Over The Weekend: Ulivutiwa na nini hasa katika utendaje wake?

Belle: Alikuwa mchapakazi. Si mvivu wala mwepesi wa kukata tamaa. Nakumbuka kuna siku tulienda ku-shoot kwenye ofisi ya Adamu Juma, nakumbuka tulikaa pale mpaka usiku, lakini Agnes hakulalamika.

Over The Weekend: Nini hasa kilimfanya Agness ajulikane zaidi kupitia jina la Masogange?

Belle: Nafikiri ni kutokana na wimbo wenyewe kuwa mzuri, video nayo ikawa kali na kuanzia hapo kila mtu akamjua Agness kwa jina la Masongange.

Over The Weekend: Ulizipokeaje taarifa za msiba na ulizipata saa ngapi?

Belle: Kiukweli nilizipokea katika hali ambayo siyo nzuri hata nashindwa kuelezea kwa sababu kuna mtu alinipigia simu akiwa kama ananiulizia hivi, ilikuwa muda wa saa kumi jioni, mimi nilishangaa kwa sababu nilikuwa nimekaa tu mahali tunapiga stori, nikiwa Iringa kwa ajili ya masuala ya kifamilia zaidi. Nikajua tu kama stori tu si unajua kuna ile mtu kuzushiwa tu kama fulani kafa, lakini inakuwa siyo kweli kama kipindi kile ilivyokuwa kwa Mzee Mjuto…

Over The Weekend: Enhe! Ulithibi-tishaje sasa kama ni kweli amefariki dunia?

Belle: Wakati nikiwa bado ninatafakari na kuamini kuwa ni uzushi tu, mara kuna mtu mwingine tena akanipigia, ikabidi mimi nimpigie simu dada yake, Agness, lakini simu haikupokelewa, basi ikabidi niingie kwenye mitandao ya kijamii nikakuta watu wanne hivi wameweka, basi nikaona tu niamini kwamba hatuko naye tena.

Ikabidi nilipokee kwa sababu mimi mara ya mwisho nilikuwa na taarifa za kuhusu mahakamani, lakini kuhusu ugonjwa, sikuwa najua, lakini dah naumia sana kuhusiana na hili.