F Mlinga akosoa vazi la mwanamke katika Nembo ya Taifa | Muungwana BLOG

Mlinga akosoa vazi la mwanamke katika Nembo ya Taifa


Mbunge wa Ulanga kwa tiketi ya CCM, Goodluck Mlinga ameiomba Serikali ipige marufuku matumizi ya nembo ya Taifa yenye picha ya Bibi na Bwana kwa sababu mwanamke huyo amevaa wigi hivyo kutoakisi maisha ya Mtanzania.

Mbunge huyo ameomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ambapo amedai katika nembo hiyo kuna Bwana amevaa lubega ambaye anaakisi maisha ya Mtanzania lakini kwa Bibi sivyo.

“Bibi aliyevaa wigi haakisi maisha halisi ya Mtanzania hivyo naiomba Serikali isitishe matumizi ya nembo hiyo na izuie isitumike hadi ifanyiwe marekebisho kwani bibi amevaa wigi ambalo haliakisi maisha ya Mtanzania,” amesema Mlinga.


Akijibu mwongozo huo Chenge alihoji iwapo tukio hilo limetokea leo hadi Mbunge huyo anakauliza na kwa vile halijatokea leo halipo kwenye kanuni. Pia amesema kwa sasa wanatakiwa kuheshimu sheria inayosimamia nembo.

Utakumbuka May 13, 2016 Mhe. Mlinga alisimama Bungeni na kusema kwa namna msanii Diamond Platnumz anavyoiwakilisha nchi vizuri kimataifa anastahili kujengewa sanamu na kupendekeza kuwekwa katika mnara wa askari.

“Ingekuwa amri yangu tungechonga sanamu la Diamond tukaliweka kwenye mnara wa Askari, ule mnara tumeuchoka. Ametufikisha mbali na ameitangaza nchi yetu huko mbele” alisema na kuendelea.

“Serikali hatuna mpango wowote wa kuwasaidia wanamuziki, wanapenya wenyewe tunaenda kukutana nao mbele na sisi tunajifanya kuwasaidia. Yuko wapi Mr. Nice, Saida Karoli aliyenichambu kama karanga?, hatujawawekea mfumo mzuri, ninaongea haya nikiyamaanisha,” alihoji.