Wakulima wa kahawa waiomba Serikali kuwafadhili mbolea

Wakulima wa zao la kahawa wilayani Tarime katika Mkoa wa Mara wameiomba serikali kuwafadhlii mbolea ya kupandia na kukuzia mazao kwa lengo la kupata mavuno mengi yenye ubora.

Akiongea leo  mbele ya Wajumbe wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB)  kwa niaba ya wakulima kutoka Kijiji cha Getenga Kata ya Mbogi wilayani hapa, David Heche alisema kuwa wakulima wa zao la kahawa wilayani Tarime wanapata mavuno machache kwasababu ya hawatumii mbolea.

"Sisi wakulima wa kahawa tunapata mavuno kiduchu kwasababu hatuna mbolea ya kupandia na kukuzia kwa hali hiyo tunaomba serikali yetu itusaidie msaada wa mbolea ili tujikwamue na mavuno kiduchu ya zao hili la kahawa,"alisema Heche.

Heche aliongeza kuwa kutokana na mavuno kidogo wanayopata wakulima baadhi yao wametishia kukata miche ya kahawa mashambani huku wakidai kuwa zao hilo haliwapatii fedha ya kutosha kuendeshea maisha ya familia.

Naye Ibrahimu Chacha Burure alisema kuwa wakulima wa kahawa wa Tanzania wanakumbwa na changamoto  ya wakulima kutoka nchi jirani ya Kenya kuja kuuza hapa kahawa yao isiyokuwa na ubora na kusababisha bei ya kahawa Tanzania kushuka sokoni.

Mkulima Burure alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali ya Tanzania kujali wakulima wake kama nchi ya Kenya kwa kuwafadhili mbolea pamoja na mikopo.

Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Kahawa na Uendeshaji Bodi ya KahawaTanzania (TCB), Kajiru Kisenga alisema kuwa serikali imepanga utaratibu mzuri kipindi hiki cha uongozi wa Awamu ya Tano juu ya zao la kahawa ili kuwapatia wakulima fedha nyingi tofauti na hapo nyuma.

Kisenga aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kwanza imepiga marufuku waachuuzi wa kahawa ambao walikuwa wanawaibia wakulima kununua kwa kutumia vipimo vya Gorogoro badala ya kutimia mizani ambayo imekaguliwa.

"Serikali imetoa maelekezo ya kuuza kahawa kwa wakulima kuwa kila mkulima anatakiwa kuuza kahawa yeke kwenye chama cha msingi na kuwa chama hicho kitakuwa kinanunua kwa kilo kahawa yote ili kuondokana na suala zima la kuwapunja wakulima,"alisema Kisenga.

Afisa Masoko Rogatus Meela pamoja na Desder Mboya waliwataka wakulima kuandaa kahawa kwa ubora ili kupata mavuno mengi pamoja na bei nyingi ili kupata fedha ya kutosha katika matumizi ya kifamilia.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia