F CRDB yatangaza kuongeza mkopo hadi milioni 100 | Muungwana BLOG

CRDB yatangaza kuongeza mkopo hadi milioni 100


BENKI ya CRDB imetangaza kuongeza kiasi cha mkopo kwa wafanyakazi kutoka Sh. milioni 50 hadi Sh. milioni 100 ambayo itatolewa ndani ya siku moja, huku muda wa kurejesha ukiongezwa kutoka miaka sita hadi saba.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei alisema pia benki hiyo imepunguza riba ya mikopo hiyo kutoka asilimia 22 hadi 16, ili kuwezesha wafanyakazi kukopa kwa wingi.

Alisema kiwango cha chini cha mshahara kupata mkopo ni Sh. 200,000 na kwamba punguzo la riba litawanufaisha watumishi wote - sekta ya umma na mashirika na kampuni binafsi.

Dk. Kimei alisema benki hiyo imeamua kupunguza riba ili kutoa unafuu na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wateja wake na Watanzania kwa ujumla, ili kusaidia kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

"Riba katika mikopo imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wateja hivyo kusababisha wengi wao kuogopa kukopa," alisema Dk. Kimei lakini "leo hii nina furaha kuwatangazia kuwa kile kilio cha muda mrefu sasa tumekipatia suluhisho kwa kupunguza riba kwa mikopo ya wafanyakazi kutoka asilimia 22 iliyokuwa ikitozwa hapo awali hadi kufikia asilimia 16."

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema benki hiyo imeanzisha utaratibu wa kununua mikopo kwa wateja ambao wamekopa katika taasisi na benki nyingine ili kuwapa fursa ya kukopa CRDB.

Kuhusu faida ya kupungua kwa riba hiyo, mkurugenzi huyo alisema itaongeza mzunguko wa fedha kutokana na kupungua kwa gharama ya mikopo na hivyo kuchochea kukua kwa uchumi.

Kwa mujibu wa Dk. Kimei, faida nyingine ni kuongeza kiwango cha ukopeshaji hivyo kuongeza kipato na mitaji ili kuchochea shughuli za maendeleo, kuongeza uwezo wa manunuzi ya wananchi, jambo ambalo litachochea uzalishaji na ukuaji wa sekta ya viwanda, kupunguza kiasi cha makato ya kila mwezi kwa wakopaji.

Alisema pia itasaidia kuendana na sera ya serikali ya kutaka kupunguza viwango vya riba za ukopeshaji na hivyo kusisimua shughuli za kiuchumi nchini

Kimei ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki nchini, aliziomba Benki Kuu (BoT) na Tume ya Ushindani (FCC) kufuatilia kwa karibu baadhi ya benki ambazo zinawakandamiza wafanyakazi kwa kuwawekea vigezo na masharti magumu hasa pale wanapotaka kuhama kwenda benki nyingine yenye masharti na riba nafuu.

BENKI NMB
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Benki ya NMB nayo ilitangaza kupunguza riba, kutoa mikopo ya mpaka Sh. milioni 150 kwa wafanyakazi nchini ndani ya saa 24 na kuongeza muda wa marejesho kufikia miaka sita.

NMB imepunguza riba kutoka asilimia 19 hadi 17.

Mikopo hiyo haibagui wafanyakazi wa sekta binafsi au serikali sharti kuu likiwa mikataba ya kudumu au ya muda mrefu.

Kutolewa kwa mikopo hiyo ni mwendelezo wa sekta ya benki nchini kutoa mikopo ya kima kilichoongezeka, masharti nafuu, huku riba za benki zikipungua kwa viwango tofauti tofauti.

Awali kupata mkopo benki ndani ya siku saba za kazi ilionekana kuwa muda mfupi zaidi nchini, lakini sasa muda huo umefyekwa kwa asilimia 90 na CRDB na NMB.

Aidha, mapema mwezi huu Bank Of Africa Tanzania (BOAT) ilitangaza neema kwa watumishi wa umma baada ya kushusha riba ya mikopo kwa kada hiyo kutoka asilimia 14 hadi 11.

Aidha, benki hiyo imepunguza masharti ya ukopaji huku muda wa urejeshaji ukiwa ni mpaka miaka mitano.

BOAT ilisema uamuzi huo umetokana na hali ya soko la ushindani kimabenki iliyopo sasa na nia ya kuongeza wigo na upatikanaji wa mikopo kwa wafanyakazi wa serikali.

Kumekuwa na ushindani mkali katika sekta ya benki katika miezi ya karibuni, nyingi zikishindana kuboresha huduma ambazo mwaka mmoja tu uliopita zilikuwa nadra kutolewa ama zikipatikana kwa masharti magumu.

Kwa mujibu wa BOAT, mikopo yake itaanzia Sh. milioni moja hadi Sh. milioni 30 na kwamba ipo katika mkakati wa kufikisha Sh. milioni 50 kama kima cha juu, na mkopaji atapewa kadri ya mshahara wake unavyoruhusu.

Desemba 13, mwaka jana mjini Dodoma Rais John Magufuli alizitaka benki kuangalia uwezekano wa kupunguza riba ya mkopo huku akiipongeza CRDB kwa kuunga mkono sera ya viwanda.

RIBA IMESHUKA
Akizungumza wakati wa Mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) mapema mwaka huu kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki, Dk. Kimei alisema riba ya mikopo katika benki za biashara nchini imeshuka kwa asilimia 16.

Dk. Kimei alikuwa akitoa ufafanuzi wa hoja za wafanyabiashara kuhusu kiwango kikubwa cha riba za mikopo katika benki.

Mkutano huo uliwakutanisha wafanyabiashara wakubwa kutoka mikoa 26 nchini, ambao walieleza kero na matatizo wanayokutana nayo kwa mwenyekiti wake Rais John Magufuli na kuomba zitatuliwe.

“Riba za mabenki zitashuka hadi asilimia sita, sekta binafsi zitapata mikopo hadi asilimia 11, lakini hazitashuka kwa mara moja,” alisema Dk. Kimei.

Dk. Kimei ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB alisema sababu kubwa iliyokuwa ikisababisha uwapo wa riba kubwa kwa wafanyabiashara ni Benki Kuu (BoT) kutoza riba kubwa kwa benki pindi zinapokopa kwake.

Hata hivyo, Rais John Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa Baraza hilo alisema zamani benki ziliweka riba kubwa kwa sababu zilikuwa zikifanya biashara na serikali.

Alisema serikali ndiyo ilikuwa ikikwamisha kushuka kwa riba kwa sababu kulikuwa na maofisa waliokuwa wanapanga njama kwa kuingia makubaliano na benki kwa kupeleka fedha za serikali kwenye akaunti ya muda maalum, na riba itakayopatikana kuingia mifukoni.