5/16/2018

Je, ni sahihi kufunika au kukiacha kidonda wazi?

Mara nyingi ukipata jeraha au kidonda utaambiwa ukiache wazi ili kipate hewa safi hasa kama kidonda ni kibichi na kuamini kuwa njia hiyo hukifanya kipone haraka. Lakini ukienda hospitali na kidonda kibichi, jambo la kwanza ambalo Muuguzi atafanya ni kukisafisha kidonda na kukifunika au kukifunga. Kwanini anafanya hivyo?

Mwili wa binadamu ni kama mashine, lakini utofauti wake ni kwamba umeumbwa kwa miunganiko ya biolojia. Ina njia mbalimbali za kukabiliana na majeraha lakini njia ambayo imezoeleka kukitibu kidonda ni utengenezaji wa gaga (scab).

Mchakato wa kutengeneza gaga unaanza muda mfupi baada ya kupata jeraha na damu zinapotoka. Chembechembe nyeupe damu ambazo ni mahususi kuzuia uvujaji wa damu hujikusanya pamoja kwenye eneo lenye jeraha (ulipojikata, mchubuko au alama ya kipigo) na kuganda juu ya ngozi.

Gaga ni ulinzi asilia dhidi ya vimelea vya wadudu lakini kiukweli sio njia nzuri ya kutibu kidonda. Gaga linahatarisha mchakato wa uponyaji kwa kuweka kizuizi cha ukavu na seli zilizokufa. Ngozi yenye afya inatakiwa ifanye mchakato yenyewe ndani kwa kuunda tishu mpya ili kuziondoa seli zilikufa na kuharakisha uponyaji. Kukiacha kidonda wazi eti kipate hewa, sio wazo zuri hasa kama kinavuja damu.

Ikiwa kidonda kibichi kikifungwa au kufunikwa, kinaepusha seli za ngozi kukauka na kutengeneza gaga, jambo linalopunguza uwezekano wa kupata kovu kwenye eneo la kidonda. Kukifunga kidonda kuna faida nyingi ikiwemo kutunza unyevunyevu ambao unasaidia uponyaji mzuri wa ngozi, kuzuia vimelea vya wadudu, vumbi, uchafu na maji kukutana na jeraha.

Zaidi, ni rahisi kwa gaga lililofunika kidonda kutoka na kupelekea kujitonesha na kuibua jeraha tena. Kinyume chake bendeji au kitambaa kinaongeza ulinzi kwenye kidonda. Pia inakukinga kujiumiza tena. Kwa vyovyote vile, ni muhimu kukifunika kidonda kwasababu inasaidia kukilinda na inaharakisha mchakato wa uponyaji.