CUF yasisitiza maandamano mikoa ya Kusini


Chama cha Wananchi CUF kimesema kuwa endapo Serikali haitowalipa wakulima wa korosho kutoka mikoa ya kusini fedha zao za mazao kiasi cha Sh Bilioni 211 basi kitaungana na wananchi wa mikoa hiyo pamoja na madiwani na wabunge wake kufanya maandamano ya amani.

Wiki iliyopita katika Bunge la bajeti linaloendelea hivi sasa bungeni Dodoma, Mbunge wa Kilwa na Mwenyekiti wa wabunge wa mikoa ya kusini, Seleman Bungala maarufu Bwege aliiambia Serikali kuwa endapo mwaka wa fedha utaisha bila wakulima hao kurejeshewa fedha zao basi ataongoza maandamano ya amani.

Akizungumza leo na wandishi wa habari, Julius Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wakati akifanya tathimini ya bajeti ya mwaka huu alisema chao cha CUF kinasikitika kuona namna ambavyo Serikali inaendelea kuwahadaa wananchi kwa kuwaongopea kuwa uchumi unapanda ilihali kuna mambo mengi ambayo yanakwamisha maendeleo ya wananchi.

" Bajeti ya mwaka huu ukiangalia haina tofauti na ya mwaka jana, suala la ajira Serikali ndio imegoma kulitolea ufafanuzi kabisa, fikirieni kila mwaka vijana wanaomaliza elimu zaidi ya laki tisa wanaingia katika soko la ajira lakini ajira zenyewe hakuna, hawa vijana wanazidi kujaa mitaani Magufuli anapaswa kujua kuwa anatengeza bomu ambalo litakuja kulipuka tu.

" Wakulima wanalia nchi nzima, fikiria zao la korosho ambalo linawaingizia kipato kundi kubwa la wananchi wa Kusini ndio hilo ambalo Serikali haitaki kuwalipa fedha zao Bilioni 211 na sisi tumeshawaagiza wabunge wetu kupitia kwa Mwenyekiti wao (Bwege) kuhakikisha wanalipigia kelele suala hilo na Serikali isiposikia tutatoa baraka zetu kama chama kuhamasisha maandamano ya amani kwa wananchi wa Kusini kudai fedha zao," amesema Mtatiro.

Kuhusu ni wapi ambapo fedha hizo zimeenda, Mtatiro amesema Serikali imeziiba kama ambavyo imekuwa kawaida yake kufanya hivyo, " Hili la Bilioni 211 ni kama ile Trilioni 1.5 ilivyopotea bila taarifa, wanatuibia tu wanaenda kujenga uwanja wa ndege sehemu kama Chato ambako hakuna mtu yeyote anaweza kwenda," amesema Mtatiro.