6/13/2018

Hakimu akubali maelezo kesi ya kigogo wa Takukuru


UPANDE wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji na kumiliki utajiri kuliko kipato chake inayomkabili, aliyekuwa Mhasibu wa Takukuru Godfrey Gugai na wenzake umeieleza Mahakama kuwa, uchunguzi umeonesha kuwa, Gugai alifanya miamala ya uongo ili kuficha umiliki wa mali zake.

Hayo yameelezwa leo mahakamani hapo wakati watuhumiwa hao wakisomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo wamekubali maelezo yao binafsi na kuyakana mashtaka yote yanayowakabili.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.Washtakiwa wamesomewa maelezo hayo leo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi na Wakili wa serikali Awamu Mbagwa.

Akiwasomea PH washtakiwa hao, wakili Mbagwa alidai kuwa Gugai anakabiliwa na makosa mbalimbali ikiwamo kumiliki mali isiyoelezeka, kughushi na kutakatisha fedha ambayo anadaiwa kuyatenda kati ya mwaka 2005 na mwaka 2006.Alidai kuwa Gugai aliajiriwa na Takukuru kama mchunguzi daraja la tatu mwaka 2001 na baadae 2009 aliteuliwa kuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru kazi alïyoendelea nayo hadi Agosti 2016 alipofukuzwa kazi.

Alidai washtakiwa wenzake wote ni marafiki zake wa karibu na kwamba katika kipindi chote cha ajira Gugai hakuwa na chanzo cha mapato ambacho kingeweza kumpatia kipato zaidi ya ajira yake.Alidai kwenye mishahara ya mshtakiwa na malupulupu mengine alijipatia kipato halali cha Sh.852,183,160.46 kutoka kwa mwajiri wake.