Mexime atoa siri ya Kaseja kuondoka


Kocha wa Kagera Sugar Meck Mexime, ameweka wazi sababu za aliyekuwa mlinda mlango wa timu hiyo Juma Kaseja kuondoka na kutimkia KMC ya Kinondoni kwaajili ya kuitumikia msimu ujao.

Mexime amesema ni suala la maslahi ndio limemwondoa Kaseja huku akikiri kuwa walikuwa wanamhitaji sana ila soka ni biashara na mchezaji lazima afuate pesa nzuri.

''Ni kweli ameondoka, lakini amekuwa muungwana maana ameaga vizuri na kutueleza kuwa maslahi aliyopewa na Kinondoni Municipal Council FC ni mazuri hawezi kuyaacha hivyo tunamtakia kila la kheri tutajipanga na wengine'', amesema.

Mkataba wa Kaseja na KMC bado haujawekwa wazi ni wa muda gani. Kaseja ameitumikia Kagera Sugar kwa msimu miwili na sasa ataungana na kocha mpya wa KMC Mrundi Etienne Dayiragije ambaye aliachana na Mbao FC katikati ya msimu uliopita.

Kaseja bado anakumbukwa na mashabiki wa klabu ya Simba kwa kuwanyima walau nafasi ya kusawazisha kwenye mchezo wa ligi kuu kati ya Kagera Sugar na Simba uliopigwa uwanja wa taifa ambapo Kaseja alipangua penati ya Emmanuel Okwi na kufanya timu yake ishinde bao 1-0.