Mkutano wa Waziri Mkuu waua watu wawili


Maafisa nchini Ethiopia wamesema kuwa watu wawili wamepoteza maisha na wengine kadhaa wamejeruhiwa, baada ya mlipuko wa bomu kutokea kwenye mkutano wa kisiasa wa Waziri mkuu, Abiy Ahmed.

Bwana Abiy amelitaja shambulio hilo kuwa ''jaribio lililoshindwa la vikosi ambavyo havitaki Ethiopia iungane''.

Kiongozi huyo aliondolewa mara tu baada ya mlipuko, unaoelezwa wa guruneti linaloaminika kurushwa kati ya maelfu ya watu katika viwanja vya Meskel , mjini Adis Ababa

Naibu mkuu wa Polisi mjini humo anashikiliwa kutokana na kushindwa kusimamia hali ya usalama katika eneo hilo.

Maafisa wa polisi wanane wanashikiliwa na wakihojiwa kwa kushindwa kulilinda eneo lilofanyiwa mkutano

Waziri wa afya nchini Ethiopia aliandika kwenye akaunti yake ya twitter kuwa watu wawili wamepoteza maisha na wengine 44 wako hospitalini, watano kati yao wakiwa na hali mbaya sana.

Abiy alikuwa Waziri Mkuu baada ya mtangulizi wake Hailemariam Desalegn bila kutarajiwa kujiuzulu mwezi wa Februari.

Pia ni Kiongozi wa kwanza kutoka jamii ya Oromo, jamii ambayo imekuwa ikiipinga serikali kwa karibu miaka mitatu, maandamano ambayo yalisababisha mamia ya watu kupoteza maisha

Tangu ameingia madarakani amekuwa akifanya mabadiliko kadha wa kadha, ikiwemo kufungulia mitandao na chaneli za televisheni zilizokuwa zimefungiwa.