F Wadada wanaouza miili wapatiwa mtaji kuachana na biashara hiyo | Muungwana BLOG

Wadada wanaouza miili wapatiwa mtaji kuachana na biashara hiyo

Na James Timber, Mwanza
Baadhi ya watoto wa kike wanaojiuza wamepewa  mafunzo pamoja na  kuingizwa kwenye vikundi ambavyo vitawasaidia  kupata mitaji itakayosaidia kuanzisha biashara iliyo halali na  kuachana na shughuli wanazofanya za kuuza miili.

Akizungumza na Muungwana Blog Meneja Mradi wa Shirika la Cheka Sana Catherine Kalokola linalojihusisha na watoto, vijana wanaoishi katika mazingira magumu jijini Mwanza, amesema kuwa lengo kubwa ni kuwabadili vijana wa kike  na kiume kwa kuwatoa katika makundi mabaya sambasamba na kuwapa mafunzo yatakayo wabadili tabia.

"Utafiti unaonyesha wadada wanaojiuza zaidi ya asilimia 80 ambao wako kwenye hiyo biashara wameletwa na wanakuja mjini kwa kudanganywa watapata kazi labda za nyumbani lakini inakuwa ni tofauti na yule aliyemleta anakuwa anachukua asilimia flani ya fedha inayotokana na biashara hiyo kwa sababu anaishi kwake," alisema.

Amesema kuwa mpaka sasa wana vikundi nane ambapo vinne ni vya  kike na vikundi vinne ni vya vijana wa kiume ambao wako katika mazingira magumu na vikundi viwili kati ya vilivyo mtaani ndio wapo kwenye hatua ya kupatiwa mtaji na kuwezeshwa.

Pia kwa mwaka jana utafiti ulionyesha kuna jumla ya watoto na vijana 276 wapo Mwanza Mjini na shughuli wanazofanya ni za kuhama kama kuuza karanga na tumegundua watoto hao ni wasafi jambo linalopelekea kutopata idadi kamili  pale tunapo hesabu na wanaofanya kazi za kujiuza ni asilimia 26 na wanao omba ni asilimia nne pekee.

Aidha amesema kuwa katika kituo chao kilichopo Iloganzala ambacho kina jumla ya watoto 37 wanafundisha watoto kwa kushirikiana na familia yake mpaka pale atakaporekebika huku akieleza changamoto ni pale mzazi anapompeleka mtoto shule za malezi na makuzi akiwa na umri mdogo ambapo katika umri huo mtoto anafaa acheze nyumbani ikiwa ni pamoja kuzoeana na wazazi kwani hawajakomaa kiakili.