Na John Walter-Babati
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Qash, Yohani Amani Konki (18), aliyeuawa na wenzake kwa madai ya kuiba simu baada ya kwenda kwa mganga, amezikwa leo nyumbani kwao Kijiji cha Tsamas, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.
Ibada ya mazishi imeongozwa na Mwinjilisti Daudi wa Kanisa la KKKT, ambaye amewataka wazazi na walezi kurejea kwenye malezi ya kiimani na kuwakumbusha watoto kuhudhuria nyumba za ibada ili kuwa na hofu ya Mungu mioyoni mwao.
Msemaji wa familia, Aiman Konki, ameilaumu shule kwa kushindwa kuwa na ulinzi madhubuti, kwani tukio hilo lilitokea usiku shuleni hapo.
Amesema Yohani alikuwa kitinda mimba na mwanafunzi mwenye akili na nidhamu, si tu shuleni bali pia nyumbani.
Aidha, amesema marehemu alikuwa mjasiriamali mdogo aliyekuwa na bustani ya migomba iliyostawi, ishara ya kujituma kwake.
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Ibrahim Mbogo, amesema serikali ipo bega kwa bega na familia tangu msiba ulipotokea Agosti 16, 2025, ikiwemo kugharamia baadhi ya shughuli za mazishi.
Mbogo amesisitiza kuwa mganga aliyehusishwa na tukio hilo ambaye alikimbia, atakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Mamia ya wananchi wamejitokeza kushiriki mazishi hayo huku wakitoa wito kwa serikali kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake dhidi ya wahusika.
0 Comments