7/11/2018

Croatia, England kukipiga kwenye uwanja huu


Croatia itavaana na England katika Uwanja huu.

Unakumbuka mechi ya fainali ya vilabu bingwa ulaya 2008 kati ya Manchester United na Chelsea ambayo United ilishinda kupitia mikwaju ya penalti? Basi huu ndio uwanja ulioandaa ngarambe hiyo.

Kubwa zaidi ya viwanja vyote, Luzhniki, ulioko Moscow, Ulifunguliwa 1956 kabla ya kukarabatiwa na kuzinduliwa tena 2018.

Historia yake:

Uga wa Luzhniki ​​ulifahamika kama uwanja wa Central Lenin. Ulijengwa ndani ya siku 450 kati ya 1955 na 1956 - kuashiria azma ya serikali ya Kisovieti baada ya wanariadha wake kurejea kutoka mashindano ya Olimpiki,Helsinki 1952, wakiwa na medali 71.

Uwanja huu umekuwa na furaha na majonzi.

Licha ya kuwa mwenyeji wa Olimpiki 1980 na kuwalaki zaidi ya mashabiki 100,000, miaka miwili baadaye, watu 66 walifariki wakati mashabiki walipokuwa wakiwania kutoka nje kwenye finali ya kombe la UEFA kati ya Spartak Moscow na waholanzi HFC Haarlem.

Umewahi kuandaa fainali ya kombe la UEFA 1999 ambapo Parma iliilaza Marseille. Uwanja huu utakuwa wa tano kuandaa mechi ya fainali ya kombe la dunia, fainali ya kombe la Vilabu bora Ulaya, pamoja na mashindano ya Olympiki.

Usisahau, mmoja kati ya hawa atarejea hapa kwa minajili ya kucheza fainali Jumapili, 15 Julai.