7/11/2018

Mvuto wa Okwi, Bocco wachangia mapato ya Simba kuwa juu


INAELEZWA kuwa, kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mashabiki wengi waliingia uwanjani na kushuhudia mechi za Simba kutokana na mvuto waliokuwa nao washambuliaji Emmanuel Okwi na John Bocco.

Simba ndiyo timu iliyoweka rekodi msimu uliopita kwa kutazamwa na mashabiki wengi zaidi kuliko timu nyingine zote hali iliyoifanya kupata mapato mengi zaidi.

Okwi na Bocco kwa pamoja walikuwa chachu ya mafanikio ya Simba kwa msimu uliopita na kuchangia timu hiyo kutwaa ub¬ngwa wao wa 18.

Mvuto wa wachezaji hao ambao kwa umoja wao walifunga mabao 34 kati ya 62 yaliyofungwa na Simba kwa msimu mzima, uliwafanya mashabiki wengi kuingia uwanjani kuangalia mechi 30 za timu hiyo kwa msimu uliopita ambapo walishinda michezo 20 kati ya 30 na kutoka sare mechi tisa. Mechi moja pekee ndiyo walipoteza mbele ya Kagera Sugar.

Kwa mujibu wa takwimu za mapato kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kutoka Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Simba walikusanya jumla ya Sh 380,867,592 kwa msimu mzima huku wapinzani wao Yanga wakishika nafasi ya pili kwa kukusanya Sh 257,113,365.

Lipuli FC ya Iringa yenyewe iliingiza Sh 71,908,665 na kushika nafasi ya tatu, Singida United iliingiza Sh 68, 939,621 na kushika nafasi ya nne.

Nafasi ya tano, imeshikwa na Mbeya City ikiwa imeingiza Sh 54,766,008, Mbao FC ya sita Sh 51,719,270. Saba ni Majimaji Sh 49,377,409, nane Azam FC Sh 45,286,214, tisa Ndanda Sh 42,951,351, kumi Kagera Sugar Sh 40, 756, 536.

Njombe Mji ya 11 Sh 40,637,642, Stand United ya 12 Sh 36,126,778, Mtibwa Sugar ya 13 Sh 33,557,913, Prisons ya 14 Sh 28,580,829, Ruvu Shooting ya 15 Sh 19,774,569 na Mwadui FC ya mwisho Sh 19,135,116.