Sababu Nne (4) Kwa Nini Hutakiwi Kujilinganisha Na Watu Wengine


Hapo ulipo hebu jiulize swali hili? Bado unaendelea kujilinganisha na watu wengine? Inawezekana ukawa unajilinganisha na watu wa familia yako, rafiki zako au jirani zako. Tabia hii ya kujilinganisha ipo sana kwa wengi.

Kwa bahati mbaya sana tabia hii ya kujilinganisha chanzo chake kikubwa kimeanzia tokea ukiwa mtoto. Ukiwaangalia watoto wanajilinganisha sana na wenzao kwa mambo mengi kama kwenye mavazi waliyonayo, midoli wanayochezea, nyumba wanayoishi na vinginevyo.

Kwa sababu hiyo hujikuta inapelekea unapokuwa mtu mzima unaanza kusema siwezi hiki au siwezi kile au mimi si bora katika jambo lile, lakini hapa unaona yote hiyo inatokana na  kujilinganisha. Tabia hii ya kujilinganisha kwa maendeleo ya mafanikio yako si nzuri.

Kivipi tabia hii si nzuri ya kujilinganisha na wengine, zifuatazo ni sababu za msingi ambazo unatakiwa ujue kwa nini kujilinganisha hakufai.

1. Kujilinganisha na wengine, inakupozea furaha yako.
Kwa jinsi unavyozidi kujinganisha na watu wengine, hiki ni kitu ambacho kitakupotezea furaha yako pasipo kujua. Kuna maeneo ambayo unatakuwa unajiona hufai ama umepungukiwa vitu fulani hivi kwa sababu ya kujilinganisha.

Siri ya kuweza kudumisha furaha yako, acha kujilinganisha sana na watu wengine. Ishi maisha yako na kimbia mbio zako mwenyewe ambazo utaziona mbio hizo zitakusaidia kuweza kufanikiwa na kufikia mafanikio yako makubwa.

2. Kujilinganisha na wengine, inakuzuia usisonge mbele sana.
Unapokuwa unajilinganisha na watu wengine badala ya kuweka juhudi za kukusaidia kusonga mbele, juhudi hizo unazimaliza kwa kujilinganisha. Matokeo yake unajikuta unadumaa badala ya kusonga mbele sana unaishia palepale.

Hata ikitokea unajilinganisha na wengine na ukafanikiwa kusonga mbele, pia hutasogea sana, badala yake utajikuta unaishia katika eneo lile lile  ambalo wale unajilinganisha nao wamefika katika eneo hilo.

3. Kujilinganisha na wengine, hakuwezi kukubadili wewe.
Kuna watu ambao wanakuwa wanajilinganisha sana katika eneo la sura, hasa kwa wanawake. Hata ukijilinganisha vipi, lakini elewa utabaki wewe kuwa wewe. Hakuna kitakachobadilika, hautaweza kubadili sura yako.

Kama unajilinginisha kwa hivi, unatakiwa kujua unajipotezea muda. Kazana na mambo yako na usiendelee na mambo ya wengine au uzuri wao. Kazana  sana kubadili yale yaliyo yako na si kukazana kujibadili wewe kupitia wengine ni hatari kwako.

4. Kujilinganisha na wengine, kunakupotezea ubora wako.
Utaupata ubora wako na utaboresha maisha yako, kama unakazana kuwa bora wewe kuliko ilivyokuwa jana yako. Kujilinganisha na wengine utajipotezea sana ubora wako, maana utafanya kama wale unaojilinganisha nao na hautavuka sana.

Hizi ndizo sababu za msingi za kwanini hutakiwi kujilinganisha na wengine. Fanyia kazi sababu hizi na kuanzia sasa anza kuishi maisha yako wewe kama wewe. Ukumbuke kuendelea kujilinganisha na wengine huko ni kujipoteza.