Fey na Kiben Ten Chake watimuliwa nyumba wanayoishi


UBUYU mzuri ni ule unaopikwa kwa ustadi wa hali ya juu, yaani watu wa Pwani wanaelewa ubuyu mtamu ulivyo.

Ubuyu mtamu uliotufikia unamhusu msanii wa miondoko ya Mduara ambaye pia ni mwigizaji wa filamu za Kibongo, Faiza Omary ‘Sister Fey’.

Inadaiwa kwamba, hivi karibuni, mwanamama huyo alilimwa barua ya kuhama nyumba kutoka kwa mwenye nyumba wake baada ya kukerwa na tabia yake na kiben’teni wake aliyetambulika kwa jina moja la Eliasi anayeishi naye maeneo ya Kinondoni, Dar.

Kwa mujibu wa msambaza ubuyu huo wa motomoto, awali Fey hakuwa na kiben’teni wake huyo, lakini baada ya muda ndiyo akampeleka wakawa wanaishi wote ila mama mwenye nyumba alikuwa akikereka na maisha wanayoishi kwa kuwa kuna wakati wanabebana na kupelekana bafuni, jambo ambalo aliona siyo zuri kwa watoto wanaoishi kwenye nyumba hiyo.

“Unajua awali Fey alikuwa singo kwenye nyumba hiyo, sasa alipoanza uhusiano wa kimapenzi na kiben’teni wake, ikawa ni shida maana wanaoneshana mahaba yao hadharani.

“Unaambiwa mama mwenye nyumba alikuwa anakerwa na vitendo vyao ndiyo maana wakapewa barua ya kuhama,” alisema mtoa ubuyu wetu.

Chanzo hicho kilizidi kufunguka kuwa, kuna wakati usiku Fey anaimba nyimbo za mapenzi na jamaa huyo huku wakipokezana, jambo lililosababisha usumbufu kwa majirani huku wakidaiwa kuwa na tabia ya kukimbizana usiku na kucheka kwa kuangushana kwa makelele.

“Jambo hilo kwa kweli lilikuwa ni kero ambayo mama mwenye nyumba hakuwa anaipenda kwenye nyumba yake.

“Yaani mwenye nyumba wake alipokuwa akiona vituko hivyo kuna wakati anatamani kulia kabisa kwa sababu anakaa na vijana wake wadogo wanaolingana na huyo mpenzi wake Fey,” kilizidi kumwaga ubuyu.

MSIKIE FEY

Baada ya Ijumaa Wikienda kulambishwa ubuyu huo lilimtafuta Fey na kumweka kitako kuhusu madai hao ya kupewa barua ya kuhama kutokana na kiben’teni wake ambapo alifunguka kama ifuatavyo;

Ijumaa Wikienda: Vipi Fey, kuna madai kuwa umepewa barua ya kuhama nyumba kwa sababu ya huyo kiben’teni wako. Hii imekaaje?

Fey: Unajua mimi ni mkweli sana, kwenye hilo siwezi kukataa, ni kweli nimepewa barua, lakini nimepokea kwa mikono miwili maana huyu (Eliasi) ndiye nimempenda. Mambo aliyoandika mama mwenye nyumba kwenye barua ni ya kawaida kwa wapenzi.

Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo sasa umechukua hatua gani?

Fey: Hakuna cha zaidi kwani sasa hivi tunatafuta sehemu nyingine tuhamie.

Ijumaa Wikienda: Sasa na kama huko watakuwa pia hawapendi mambo hayo itakuwaje?

Fey: Tutahama maana mimi hiyo ndiyo furaha yangu na siwezi kubadilika.

Ijumaa Wikienda: Mna mpango wa kufunga ndoa?

Fey: Ndiyo. Hivi karibuni mtasikia tu.

Baada ya kuzungumza na Sister Fey, Ijumaa Wikienda lilimgeukia jamaa huyo ili naye afunguke madai ya kumsababishia Fey kupewa barua ya kuhamishwa kwenye nyumba ambapo alisema yeye haoni kama kuna tatizo kwenye hilo ila inawezekana hapo hawakuwapenda tu.

“Unajua kwenye uhusiano wetu kuna misukosuko mingi sana, najua watu wanaumia roho, lakini Mungu ni mwema, naamini tutafika tunapotaka,” alisema Eliasi.