Mahakama yamuhukumu Mhasibu Kifungo cha Miaka Mitano Jela

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu miaka 5 jela aliyekuwa Mhasibu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama, Gryson Mnyawami baada ya kupatikana na hatia ya kosa la wizi wa zaidi ya Shilingi Milioni 9 akiwa mtumishi.

Hukumu hiyo, imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega ambapo amesema upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake 5 wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mtuhumiwa ametenda kosa la wizi.

Hata hivyo, kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Hakimu Mtega alitaka mwendesha mashtaka kueleza kuhusu kumbukumbu za mshtakiwa kama anamakosa mengine ama la.

Mwendesha Mashtaka, wakili wa Serikali, Janeth Magoha ameekeza kuwa hakuna kumbukumbu za makosa kwa mshtakiwa, hili ni kosa lake la kwanza.

“Sina kumbukumbu za mshtakiwa, ila naomba mahakama itoe adhabu kali kwa kuwa kitendo cha wizi alichofanya akiwa kama mtumishi wa umma ni kibaya, kinaitia hasara kubwa Serikali, pia suala la wizi katika Chuo cha ustawi limekuwa likitokea mara kwa mara Kitendo cha yeye kudhulumu wanafunzi siyo haki kwani ile ni hela ya walipa kodi,” alisema.

Katika utetezi wake, mshtakiwa Mnyawami, aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu, kwani awali alikubali kulipa fedha hizo taratibu lakini taasisi ndiyo ilimkatalia.

“Dada yangu ni mgonjwa na mama yangu ni mjane na wote wananitegemea,”.

Katika mashtaka yake, anadaiwa May 31, 2014 katika Chuo cha ustawi wa jamii kilichopo Kijitonyama wilayani Kinondoni mtuhumiwa akiwa ameajiriwa kama Mhasibu wa Chuo hicho aliiba sh, 9,714,000 mali ya muajiriwa wake ambayo ameipata kutokana na nafasi yake kazini hapo.