Yule mwanzilishi wa Sherehe za Simba Day, aliyekuwa mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali amefunguka kuwa siku hiyo muhimu kwa wanasimba itumike kwa ajili ya kuijenga timu hiyo ili iweze kufanya vyema katika ligi na michuano ya kimataifa kwa kudumisha upendo baina yao pamoja na umoja ili kufanya vyema ikiwa ni pamoja na kuwapongeza viongozi waliopo madarakani akiwemo Mohamed Dewji ‘MO’.
Simba inatarajia kuhitimisha sherehe za Simba Day leo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar kukipiga na Asante Kotoko ya Ghana ikiwa ni mchezo wa kimataifa wa kujipima nguvu ambapo ni sehemu ya kutambulisha wachezaji wapya wa msimu.
Dalali ikiwa ni kauli mbiu yake katika siku hiyo kwa Wanasimba, ili wawe na msimu mzuri wa ligi kuu, amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuendeleza umoja na mshikamano ndani ya timu ili iweze kuwa nzuri msimu ujao na yenye ushindani wa hali ya juu kwa kuwa wana kikosi kizuri.
“Nashukuru kuona viongozi waliopo madarakani wanaendeleza tamasha hili la Simba day, mimi nikiwa kama muasisi nawapongeza sana kwani lipo mahususi kwa ajili ya kutuweka pamoja.
“Wanasimba tunatakiwa tuungane tuwe kitu kimoja tuna timu nzuri, tusibaguane tuwe kitu kimoja ili tuweze kufanya vizuri kwenye ligi na hata michuano ya kimataifa,” alisema Dalali.
