Mabingwa wa soka nchini Simba ya Dar es Salaam leo imetambulisha rasmi benchi la Ufundi pamoja na wachezaji wake waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi kuu ya Tanzania Bara, na michuano ya kimataifa.
Utambulisho huo umefanyika mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola aliyemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo, katika tamasha la Simba day ambalo limefanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Lugola katika hotuba yake fupi amezipongeza klabu ambazo zimekuwa na mipango ya kujitafutia fedha ikiwemo kutengeneza jezi lakini akawaonya wale wote wanaokwamisha juhudi hizo kwa kutengeneza jezi feki akisema dawa yao imepatikana.
Kikosi hicho cha Simba kimejumuisha wachezaji wapya waliojiunga na timu hiyo kutoka vilabu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi pamoja na wale walioitumikia kwa msimu uliopita.
Aidha katika kunogesha tamasha hilo ambalo limetumika pia kuzindua gazeti la klabu hiyo linaloitwa Simba Nguvu Moja, timu ya Simba ikiwa chini ya Kocha wake Mpya Patrick Aussems ilicheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya Asante Kotoko ya Ghana.
Awali kabla ya tamasha hilo, Simba iliweka kambi ya mazoezi nchini Uturuki na kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.
