Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda amewashauri viongozi wa vyama vya siasa kuwa makini na matumizi ya lugha wanayotumia pindi wanapotaka kumshauri Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano Dk.John Magufuli.
Shibuda ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati viongozi wa vyama vya siasa nchini vilipokutana kwa lengo la kujadili mabadiliko ya kikatiba na kisheria kuhusu uchaguzi kabla ya Uchaguzi kuu wa mwaka 2020.
Wakati huo huo amewahakikishia kuwa Rais Magufuli hawezi kuufuta mfumo wa vyama vingi bali kilichopo anaviimarisha na kwamba ipo siku atazungumzia hilo kwa kina.
Katika mkutano huo ambao umeandaliwa na Jukwa la Katiba Tanzania (Jukata), Shibuda amesema ni vema wanasiasa wakawa makini katika matumizi ya lugha hasa kwa kuzingatia zama zimebadilika.Amesema lugha ambazo walikuwa wanazitumia katika awamu zilizopita lazima wanasiasa wajue zama hizi hazina nafasi na hivyo kushauri wachague lugha ya kusema wanapotaka kushauri au kuzingumza jambo kwa Rais.
“Kikubwa lazima tutambue kila kabila na utamaduni wake.Lugha ambazo unaweza kuzitumia kumwambia Mzaramo au Mkwere anaweza kucheka lakini lugha hiyo hiyo ukiitumia kwa Mkurya atakukata panga.“Lugha ambazo unataka kumwambia Rais wa Serikali ya Awamu Tano lazima ziwe na staha kwani kinyume na hapo anaweza kukupa jibu ambalo litakukwaza.Tukubali kuwa mila na desturi zinatofautina sana,”amesema Shibuda.
Akifafanua katika hilo Shibuda ametoa mifano kuwa hata unapotaka kwenda kuoa ukienda kutoa posa Bukoba watakwambia nenda na mkungu wa ndizi, ukienda Tanga watakwambia nenda na kuku wa kitoweo na ukienda Usukumani utaambiwa uswage Ng’ombe.“Vivyo hivyo hata unapotaka kumshauri Rais lazima uzingatie mila na desturi.Nimeona hili niwaambie kwani kuna changamoto ya matumizi ya lugha miongoni mwetu,”amesema Shibuda
