Sierra Leone yaimwagia pongezi NSSF



Sierra Leone imefurahishwa na hatua kubwa ya maendeleo yanayofanywa na mfuko wa Taifa wa Hifadhi wa Jamii NSSF nchini na kwamba italazimika kuiga baadhi ya masuala ikiwemo kuanzisha kitengo kipya cha viatarishi katika mfuko wao ili kuongeza ufanisi na kuzuia kutokea kwa majanga yanayoweza kujitokeza.

Hayo yamesema na  Naibu Mkurugenzi mkuu wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Bima Sierra Leone Mohammed Gondoe alipotembelea katika makao makuu ya NSSF jijini Dar es salaam na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii NSSF, William Erio ambapo amesema kuna mambo mazuri yamefanywa na NSSF hivyo hawana budi kujifunza.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa NSSF William Erio amesema Tanzania na Sierra Leone zitaendelea kushirikiana na kuwa na mahusiano mazuri katika kuhakikisha wanabuni mipango ya kusaidia ukuaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii ya Taifa.

Mifuko ya Hifadhi ya jamii ya nchi hizo imekuwa ikishirikiana kwa muda mrefu jambo ambalo limesaidia kuongeza ufanisi na weledi katika utendaji kazi wake kwa wafanyakazi wa mifuko hiyo.

Gondoe na wajumbe wenzake kutoka nchini Siera Leone wapo nchini kujifunza masuala mbali mbali ya hapa nchini ikiwemo mfumo wa utoaji mikopo ya elimu ya juu uliopo chini ya wizara ya elimu,sayansi na teknolojia.