Straika wa Azam FC ateswa na majeraha

MSHAMBULIAJI wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Azam FC, Mbaraka Yusuph amesema kitendo cha kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi kinamnyima raha.

Mbaraka alisema anatamani kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza ili aonyeshe uwezo wake lakini kwa sasa hali hiyo haiwezekani.

"Hakuna mchezaji anayependa kukaa benchi... naendelea kupambana na kufanya vizuri kwenye mazoezi ili nimshawishi kocha anipe nafasi kwenye kikosi cha kwanza," alisema Mbaraka.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Azam FC msimu uliopita, alisema majeraha aliyokuwa nayo yamechangia kupoteza namba kwenye kikosi cha kwanza.

"Kwa sasa nipo sawa, lakini kukaa nje kipindi kile kumechangia kushuka kwa kiwango changu lakini sasa napambana kurejea kwenye kikosi, naamini mambo yatakaa sawa," alisema mshambuliaji huyo.

Mbaraka amepoteza namba kwenye kikosi cha kwanza mbele ya washambuliaji, Tafadzwa Kutinyu na Danny Lyanga ambao wametua klabuni hapo wakitokea Singida United.

Nyota huyo hajaichezea timu yake mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu tangu ilipoanza hapo Agosti 22 mwaka huu, huku Azam ikiibuka na ushindi katika mechi zote mbili ilizocheza.
Mpya zaidi Nzee zaidi