8/10/2018

UN yailaani Saudi Arabia kuishambulia Yemen


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulizi la Alhamis la anga nchini Yemen lililofanywa na muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na kupelekea vifo vya watu kadhaa.

Guterres ametaka uchunguzi huru na wa haraka kufanywa.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, Guterres amezitaka pande zote zinazohusika katika vita hivyo vya Yemen kuchukua tahadhari sana na kuhakikisha kwamba haziwalengi raia na vyombo vya kiraia wakati wanapofanya operesheni za kijeshi.

Marekani pia imeungana na Umoja wa Mataifa katika kulaani shambulizi hilo na imetaka uchunguzi kufanywa baada ya watoto 29 waliokuwa katika basi lao la shule kuuwawa wakati basi lao liliposhambuliwa. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani Heather Nauert amesema Marekani inahuzunishwa na ripoti za shambulizi lililopelekea vifo vya raia.

Muungano wa majeshi wasema ulikuwa unawalenga waasi

"Tunautaka muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ufanye uchunguzi wa kina na wenye uwazi kuhusiana na tukio hilo. Tunachukulia kwa umuhimu mkubwa kila kisa cha mauaji wa raia," alisema Nauert. "Tunazitaka pande zote kuchukua hatua zinazostahili ili kuwalinda raia kulingana na sheria ya kimataifa na tunazitaka pande zote kuchunguza visa vyote vya mauaji vilivyoripotiwa," aliongeza msemaji huyo.

Muungano huo wa majeshi lakini umesema ulikuwa unawalenga waasi wa Kihouthi waliokuwa wamerusha kombora kusini mwa Saudi Arabia Jumatano na kupelekea kifo cha mtu mmoja ambaye alikuwa ni raia wa Yemen. Kituo cha televisheni kilicho chini ya waasi cha Al Masirah kimeonyesha picha za watoto waliojeruhiwa, nguo na mikoba yao ya shule iliyokuwa imelowa damu walipokuwa wamelala kwenye vitanda hospitalini.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba kikosi chake kiliipokea miili 29 ya watoto walio chini ya umri wa miaka 15 pamoja na watu 48 waliojeruhiwa wakiwemo watoto 30.