Chelsea na Lverpool kuvaana leo

Chelsea na Lverpool zinakutakana leo katika mchezo wa saba wa Ligi Kuu England msimu wa 2018/19, huku Liverpool ikiwa kileleni baada ya kushinda mechi zote sita, wakati Chelsea ipo nafasi ya tatu licha ya kuwa na pointi 16 sawa na Manchester City inazidiwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri, baada ya juzi kuonyesha kiwango cha juu katika raundi ya tatu ya Kombe la Ligi na kuing’oa Liverpool kwenye michuano hiyo baada ya kuifunga mabao 2-1 kwenye dimba la Anfield, leo hii ataikaribisha timu hiyo katika mechi ya Ligi Kuu England.

Chelsea inaikaribisha Liverpool kwenye dimba la Stamford Bridge katika mchezo unaovuta hisia za wengi kutokana na ubora wa vikosi vyote katika ligi msimu huu.

Ingawa Liverpool haijapoteza pointi hata moja katika ligi hadi sasa huku ikishinda mechi zote sita, mpambano wa leo unaweza kuwa wa ushindani na ufundi zaidi.

Kocha huyo raia wa Italia anayesifika kwa uvutaji sigara mfululizo, ameibadili Chelsea kiuchezaji ambayo kwa sasa inacheza soka la kuvutia la pasi nyingi huku ikipata matokeo mazuri.

Jambo jingine linaloongezea ugumu kwa Liverpool kuendeleza rekodi bora ya ushindi waliyoanza nayo msimu huu ni rekodi yao mbovu kila wanaposhuka Stamford Bridge.

Katika misimu mitano iliyopita Liverpool imeshinda mchezo mmoja wa Okoba 31, 2015, iliposhinda mabao 3-1, mechi nyingine zote imepoteza.

Ndani ya muda mfupi wa uongozi wake Sarri amefanya mageuzi yanayomtofautisha na mtangulizi wake Antonio Conte, wengi sasa wanaiona Chelsea kama mshindani wa kweli katika mbio za ubingwa.

Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, ameshaelezea kuridhishwa na mbinu za uchezaji wa timu yake.