Majaliwa atoa agizo kwa Waziri Tizeba, ataka Dodoma izalishe ufuta bora


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba kupeleka wataalamu kwenye kituo cha utafiti kilichopo Makutupora, Dodoma ili wazalishe mbegu bora za ufuta kwa ajili ya mikoa ya kanda ya kati.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Septemba 20, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mauno, wilayani Kondoa ambako alienda kukagua ujenzi wa kituo cha afya.

Alikuwa akijibu ombi la mbunge wa viti maalum, Mariam Ditopile ambaye alisema mkoa wa Dodoma ni wa pili kwa uzalishaji wa ufuta hapa nchini lakini aina ya ufuta inayozalishwa ni ya daraja la chini kwa sababu hawana mbegu za ufuta mweupe.

“Ili mradi mikoa ya kanda ya kati inazalisha ufuta, ninamuagiza Waziri wa Kilimo ahamishe watumishi kutoka kokote ili wakae Makutupora na kuwasaidia wakulima wawe na mbegu bora zenye kutoa mafuta mengi,” alisema.

Amesema kila mwaka Serikali inatumia zaidi ya dola za Marekani milioni 267 kuagiza mafuta ya kula kutoa nje ya nchi na kwamba hivi sasa imeamua kufufua mazao ya mbegu za mafuta ili mafuta ya kula yazalishwe kwa wingi hapa nchini.