Mzee mwingine wa kikombe aibuka Dar


Mamia ya wananchi jijini Dar es Salaam jana walifurika eneo la Feri kwa mtu aliyeibuka na kutangaza kugawa dawa  alizodai zinatibu magonjwa yote isipokuwa Ukimwi kwa gharama ya Sh. 3,000 kwa chupa yenye ujazo wa lita moja na nusu.

Jacob Kawawa, ambaye amesema yeye ni mganga wa tiba asilia na alianza kufanya kazi hiyo miaka 20 iliyopita lakini kwa Dar es Salaam ametoa huduma kwa miaka mitatu sasa.

Jana, mamia ya wananchi walifurika katika soko hilo kwa ajili ya kwenda kupata tiba huku wengine wakitoa ushuhuda wa kupona maradhi yaliyokuwa yakiwasumbua baada ya kuitumia.

Mashuhuda hao waliiambia Nipashe kuwa, mganga huyo alianza kutoa tiba mwezi mmoja uliopita katika eneo la Feri ingawa idadi ya wateja ilikuwa ndogo lakini mmoja wa maofisa wa soko hilo, alisema walitambua ujio wa mganga huyo juzi.

Ramadhan Omary, mchuuzi wa samaki katika soko hilo, aliieleza Nipashe kuwa alikuwa akiugua ugonjwa wa ngiri kwa miaka mingi lakini baada ya kupatiwa dawa na mganga huyo amepona.

Alisema si yeye peke yake bali watu wengi anaowafahamu waliotumia dawa hizo, wamepona magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua.

“Mimi sikufichi huyu mganga nilikuwa namwona tu hapa lakini nikawa simwelewi. Lakini baada ya kuona baadhi ya watu wamekunywa dawa zake na wakapona, wanakuja kutusimulia. Niliamua kwenda akanipa dawa nikanywa siku ya kwanza, nikarudia na siku ya pili nikapona kabisa. Nina wiki ya tatu sijaugua tena na si kawaida,” alisema Omary.

Naye kijana aliyejitambulisha kwa jina la Fadhili alidai kuwa alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya maambukizi ya njia ya haja ndogo (UTI) lakini alipotumia dawa hizo alipona kabisa.

“Sikuamini nilichukua dawa zangu na mke wangu ambaye na yeye alikuwa anasumbuliwa na UTI kila siku tukanywa mpaka leo (jana) nakwambia sijawahi kusikia maumivu ya tumbo wala mkojo kuwa mchafu,” alisema fadhili.

MSAIDIZI AWEKA WAZI
Said Mduma, ambaye ni msaidizi wake, alisema idadi ya watu wanaojitokeza kupata huduma kwa mganga hiyo inaongezeka kila siku kwa sababu ya watu waliotibiwa wakapona wanatoa ushuhuda.

“Watu waliotibiwa wakapona ndio waliojaza umati huu. Mimi ni msaidizi wake ninamsaidia kazi ya kuhakikisha usalama unakuwapo katika eneo hili, watu wapate dawa zao waendelee na shughuli zao,” alisema.

Alisema Kawawa anatoa huduma hiyo ya tiba na mke wake lakini kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu kila siku, amelazimika kuwa na wasaidizi wengi wakiwamo walinzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanaolinda eneo hilo la soko.

Alisema alikuwa akitibu peke yake kwa kusikiliza matatizo ya watu kwanza na baadaye kuwapatia dawa lakini kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu, analazimika kuwapangisha watu foleni.

“Kabla watu hawajafahamu kama dawa zake zinatibu kweli, alikuwa anakaa na mgonjwa na kuzungumza naye na ndipo anampatia dawa lakini sasa hivi watu wanapanga foleni na anatumia wasaidizi wake kuchanganya baadhi ya dawa,” alisema.

Pia alisema wagonjwa wanafika katika eneo hilo kuanzia alfajiri ingawa mganga huyo anafika eneo hilo saa 4:00 asubuhi na kuanza kuwahudumia wateja waliofika.

“Watu ni wengi kama unavyoona kuna waliofika asubuhi sana na wengine wamechelewa hivyo watu waliowahi ndio wanaanza kupatiwa dawa,” alisema Mnduma.

Alieleza na yeye alisumbuliwa na tatizo la tumbo kujaa gesi na alipotumia dawa zile alipona kabisa pamoja na kutibu tatizo la paka kuzungumza na kulia nje ya nyumba yake ambao kwa sasa hawapo kabisa.

MAZINGIRA YA KUMWONA
Nipashe ilishindwa kumfikia kiurahisi mganga huyo ambaye amezungukwa na idadi kubwa watu waliokuwa wakisuburi kupata huduma.

Mbali na wateja, pia alizungukwa na walinzi wa JKT na wasaidizi wake ambao wanamsaidia kugawa dawa na kuita wateja ambao zamu ya kupatiwa tiba imefika.

Katika eneo karibu na vizimba vya kuuzia samaki aina ya Pweza karibu kabisa na fukwe za bahari wananchi walimzunguka huku wakiwa na shauku kubwa ya kufikiwa na huduma hiyo.

Kutokana na kuwa na shauku kubwa ya kutibiwa, walikuwa wagumu kuruhusu mtu yeyote aliyetaka kupenya kwa ajili ya kumfikia mganga huyo kwa madai kuwa endapo atasumbuliwa atashindwa kufanya kazi yake vizuri na kwa wakati.

“Jamani msiende mbele mwacheni afanye kazi yake. Mtamchelewesha  muda unazidi kwenda na wengi tuko hapa tangu asubuhi,” ilisikika sauti ya mmoja wa wateja waliokuwa eneo hilo.

Katika eneo alilokuwa mganga, lilikuwa limezungushiwa kamba za manila kuashiria hakuna mteja ambaye anaruhusiwa kuvuka na kuingia ndani huku ndani kukiwa na  chupa nyingi zenye maji ya wateja zikiwa zimepangwa kwenye foleni kusubiri kuwekwa dawa.

Aidha, mganga huyo aliwapa kipaumbele wanawake wenye watoto wadogo kwa sababu hakuna eneo la kupumzikia kusubiri huduma hiyo.

NAMNA ANAVYOTIBU
Mganga huyo ambaye ni kijana, amekuwa akichukua maji makubwa ya lita moja na nusu kutoka kwa wateja na kuyamwaga kiwango cha nusu lita na yanayobaki anaweka dawa.

Dawa anazotumia ni za unga wenye rangi mbalimbali za kahawia, kijani kikavu, udongo na rangi ya njano kwa mbali ambazo akishachanganya  anampatia mteja kwa ajili ya matumizi.

Wakati wa kuchanganya dawa ndani ya maji mganga huyo anaonekana kutoongea bali kufanya kimya kimya.

 Kwa mujibu wa watu waliotibiwa, mganga huyo anatoa chupa hiyo ya dawa mgonjwa atumie mara tatu kwa siku na siku inayofuata anatoa dawa ya kurudia bure ili kukamilisha dozi.

KUFA KUFAANA
Kama wahenga wasemavyo kufa kufaana, katika eneo hilo vijana mbalimbali wanaofanya biashara ya maji ya kunywa walionekana wakihamasisha wateja kununua maji yao.

Mbali na kuuza maji pia wamekata vipande vya boksi na ‘ruber band’ ambavyo  wanatumia kumwandikia jina mteja kwenye kiboksi na kukafungua kwenye chupa ya maji ili kutochanganya dawa na kujua jina la mteja.

“Maji ya lita moja na nusu tunauza Sh. 600, kiboksi pamoja na kukuandikia jina na makapeni na kukufungua na ‘rabendi’ ni Sh. 200. Kwa hiyo tunauza kwa Sh. 800 na tukishakupa moja kwa moja unapeleka kwenye foleni,” alisema mmoja wa wafanyabiashara aliyemsihi mwandishi anunue maji hayo.

Jumanne Rashid, mfanyabiashara wa maji, alisema tangu mganga huyo aanze kutoa huduma, biashara ya maji imeongezeka na kwamba kwa siku wanauza katoni 20.

SHUHUDA
Baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo, walilieleza Nipashe kuwa, kilichowafanya wamwamini mganga huyo ni baada ya kumtibu mama aliyekuwa amepooza viungo vyake na kupona.

Mmoja wa mashuhuda hao alisema, mume ndiye aliyechukua dawa hizo na kumpelekea mke wake ambaye alipona kabisa.

“Tulimwona mama ambaye alikuja hapa anatembea anasema amepona kabisa ugonjwa wa kupooza uliokuwa unamsumbua kwa miaka mingi na alipotaka kumpa mganga fedha za shukurani Sh. 200,000 alizikataa na watu walizichukua tukagawana watu hapa tukafurahi,” alisema  shuhuda