Rais afichua siri ya kuwaachia wapinzani, akanusha kushinikizwa


Rais Paul Kagame wa Rwanda ametangaza kwamba hakushinikizwa na mtu yeyote kutoa msamaha na kumwachilia huru mwanasiasa wa upinzani Victoire Ingabire.

Akihutubia bunge baada ya wabunge waliochaguliwa hivi karibuni kuapishwa rasmi, Rais Kagame amesema msamaha aliotoa ndiyo njia aliyochagua ya kutatua matatizo na kujenga taifa hilo.

Rais Kagame amewaonya walioachiliwa huru kutuliza misimamo yao la sivyo watajikuta tena gerezani.

Miongoni mwao yupo mwanasiasa wa upinzani Victoire Ingabire na msanii Kizito Mihigo waliokuwa gerezani kwa hatia ya makosa ya uhaini.

Kiongozi huyo mkuu wa Rwanda amemuonya yeyote atakayeendelea kuwa na msimamo mkali kuwa atarudishwa gerezani.

"Hawa watu tuliowaachilia huru wakiwemo wale wanaofahamika nje kama nyota wa kisiasa, walipotoka nje walianza kupiga kelele eti 'mimi sikuomba msamaha, mimi siwezi 'na pengine kusema kwamba waliachiliwa huru kutokana na shinikizo la kimataifa.

" Shinikizo? shinikizo hapa? haiwezikani kabisa! Ukiendelea na msimamo huo unaweza kujikuta umerudi gerezani. Kama ni ushahidi wa kukuonyesha kwamba hatukushinikizwa na yeyote, unaweza kujikuta umerudi gerezani au nje ya nchi ambako utakuwa hauna kazi''.