Uchaguzi Monduli na Ukonga wawaibua Jukata, Polisi yashambuliwa


Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limelitaka Jeshi la Polisi na Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na si kutumika kisiasa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Septemba 19, 2018 na Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo amezungumzia hali ilivyokuwa katika uchaguzi wa Ubunge katika jimbo la Ukonga na Monduli pamoja na ule wa Udiwani katika kata 24.

Katika ufafanuzi wake Mwakagenda amesema amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya polisi kushangilia uchaguzi kumalizika salama wakati waliotakiwa kufanya hivyo ni wananchi.

"Polisi wanashangilia hadharani bila aibu kuwa uchaguzi umefanyika kwa amani kwani nani alitakiwa kuhakikisha kwamba amani hiyo inakuwepo si wao, wanashangilia ushindi upi wakati ni wajibu wao kulinda mali raia na mali zao”, amesema Mwakagenda.