Serikali yafunguka kuhusu matumizi ya mafuta na gesi


SERIKALI kupitia Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani inatarajia kuzungumzia mwelekeo wa nchi katika kutumia nishati ya mafuta na gesi katika viwanda.

Waziri Kalemani atatoa muelekeo huo katika Kongamano la Pili la Sekta ya Mafuta na Gesi linalotarajia kufanyika kuanzia Septemba 24 hadi 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Mbali ya Waziri kutoa mwelekeo, pia wadau muhimu wa sekta ya mafuta na gesi wakiwamo TPDC, PURA,EWURA, NEEC, ATOGS na TPSF watashiriki.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kuhusu kongamano hilo Abdulsamad Abdulrahim kutoka Shirikisho la Watoa Huduma za Mafuta na Gesi nchini amesema Serikali na wadau wa sekta ya mafuta na gesi wameunga mkono na watashiriki kikamilifu.

Amefafanua kongamano hilo limeandaliwa na Pietro Fiorentini Tanzania kwa kushirikiana na CWC Group ambapo pamoja na mambo mengine mradi wa bomba la mafuta ghafi utachambuliwa wakati wa kongamano hilo.

“Mradi huo wa bomba la mafuta unatarajiwa kuleta fursa mbalimbali katika mnyororo wa thamani.Pia kongamano hili litajadili hatua za uendelezaji wa miradi ya gesi iliyopo nchini .

“Miradi ambayo itaifanya Tanzania kuwa mzalishaji na msambazaji mkubwa wa gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki,”amefafanua.