Serikali yampa onyo la Mwisho Gigy Money


Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imempa onyo la mwisho msanii wa bongo fleva na 'video vixen' nchini, Gift Stanford maarufu kama Gigy Money kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii na endapo hatofanya hivyo basi watamchukulia sheria stahiki dhidi yake.

Hayo yamewekwa wazi na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Juliana Shonza alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv na kusema kwamba hawata waangalia usoni wananchi pamoja na wasanii kiujumla watakao kuwa wanaenda kinyumae na sheria ya mitandao.

"Huyu Gigy Money naona bado hajaacha michezo yake kwenye mitandao, safari hii sidhani kama atapona katika huu mchakato wa kuwakamata wasanii. Lakini kupona kwake labda yeye mwenyewe abadilike na awe kama sheria ya mitandao inavyotaka. Niwasii wasanii na watanzania wote kwamba waheshimu, mila na tamaduni za kitanzania kwasababu serikali ipo macho", amesema Mh. Shonza.


Pamoja na hayo, Shonza ameendelea kwa kusema kuwa "sisi kama viongozi ambao tunasimamia masuala ya sanaa, kimsingi hatuwezi kuacha hivi vitu vikawa vinaendelea kwasababu tunajua vina 'impact' kubwa kwenye jamii na kutazamwa na watu wengi na hatujui kwamba anayetazama ni mkubwa au mdogo. Kwa hiyo vitu kama hivyo vikiachwa viendelee vitakuwa na athari kubwa kwa jamii".

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema hawataacha kuelimisha jamii juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii huku akisisitiza kwamba hawasita kuwachukulia hatua stahiki watu wote wanatao bainika wameenda kinyuma na matakwa ya sheria ya mitandao.