Mkutano wa wadau wa zao la Korosho uliokuwa ufanyike leo jijini Dar es Salaam umeahirishwa ghafla bila ya kutolewa sababu za msingi na kuwaacha wajumbe wa mkutano huo kubaki wasijue nini cha kufanya.
Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kutoka katika mikoa ambayo zao hilo linalimwa wamejikuta njia panda wasijue kama waendelee kusalia jijini Dar es Salaam au kuondoka kutokana na kushindwa kupata taarifa kamili juu ya kuahirishwa kwa mkutano huo.
Aidha wabunge wengine wamesema hata kama kikao kingeahirishwa basi taratibu za kuahirisha kikao hicho zingefuatwa hata kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi na siyo kusubiri watu wafike ndio mkutano uahirishwe.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Joseph Kakunda amesema mkutano huo umeahirishwa kutokana na kujitokeza kwa kikao kingine kikubwa zaidi.
