Ambokile aanza kutajwa Simba

MSHAMBULIAJI WA MBEYA CITY ELIUDE AMBOKILE

MSHAMBULIAJI wa Mbeya City ambaye anaongoza kupachika mabao msimu huu, Eliude Ambokile, ameanza kuwa kwenye mawindo ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, imefahamika.

Ambokile amefunga mabao sita akifuatiwa na Habibu Kiyombo wa Singida United aliyecheka na nyavu mara tano, huku Meddie Kagere kutoka Simba na Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar wakiwa na mabao manne kila mmoja.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa viongozi wa Simba (jina tunalihifadhi), alisema Ambokile tayari ameshaingia katika ripoti zao kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye mechi chache za ligi ambazo zimeshachezwa.

Kiongozi huyo alisema wanahitaji kuwa na mchezaji ambaye anatimiza makujumu yake kwa zaidi ya asilimia 70, jambo ambalo Ambokile amelithibitisha.

"Ni kawaida yetu Simba na Yanga kuwahi wachezaji waliong'ara na tunafanya hivyo ili kuimarisha vikosi vyetu, ila mwisho wa siku benchi la ufundi ndio litakuwa na uamuzi wa kumsajili au kutomsajili kwa kuzingatia mahitaji yaliyoko mbele yetu," alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, Simba ina washambuliaji wengine ambao imewasajili msimu huu na bado hawajapata nafasi ya kucheza akiwamo Marcel Kaheza aliyetua kutoka Majimaji ya Songea, huku kinara wake wa msimu uliopita, Mganda Emmanuel Okwi akiwa ameanza kufungua ‘akaunti yake ya mabao wiki iliyopita.