Barcelona, Real Madrid? Naisubiri Oktoba 28


Na Tom Thomas

Oktoba 28 mwaka 1955 alizaliwa Bill Gates, kwa sasa ndiye binadamu wa pili mwenye pesa nyingi duniani, wa kwanza ni Jeff Bezos. Bill Gates anatajwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 98.

Ni pesa nyingi sana. Kama akiamua kumpatia kila mtanzania shilingi milioni mbili, bado ataendelea kuwepo kwenye orodha ya mabilionea 20 duniani.

Oktoba 28 mwaka huu, atakua akisherehekea siku yake ya kuzaliwa. Atatimiza miaka 63. Haijalishi atakua sehemu gani. Kama ni kwenye jumba lake la kifahari kule Medina, Washington au sehemu nyingine yeyote. Itakua ni siku tofauti kwake, siku ya furaha.

Wakati Bill Gates akisherehekea kutimiza miaka 63, siku hiyo ndani ya uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona, Spain kutakua na El Classico. Mechi kati ya Barcelona na Real Madrid. Ni siku ambayo wapenzi wa soka duniani watasimamisha shughuli zao kwa dakika tisini wakifutilia mechi hii.

El Classico ni mechi fulani isiyoelezeka kwa lugha ya kawaida. Baadhi ya watu wasiofutilia soka huwashangaa wale wanaoacha shughuli zao muhimu, wale wanaowaacha wake zao nyumbani kwa ajili ya kuiangalia mechi hii.

Wao huona ni kitu cha ajabu. Hawajui tu. Mechi hii hubeba hisia za mashabiki wengi. Ni mechi ambayo hutazamwa na watu wengi duniani.

Ni mechi ambayo huzalisha matukio na kumbukumbu. Usiku wa giza 'The black night' pale Santiago Bernabeu mwaka 1974. Tukio la Luis Figo kurushiwa kichwa cha nguruwe Camp Nou November 2002.

Goli la ushindi dakika za mwisho la Cristiano Ronaldo, fainali ya kombe la mfalme April 2014. Mkono wa Gerald Pique baada ya Barcelona kufunga goli la tano November 2010. Hat-trick ya kwanza ya Lionel Messi. Ni baadhi ya matukio yanayoendelea kukumbukwa.

El Classico ya March 22 mwaka 2014 ni moja kati ya mechi kali zaidi kuwahi kuzishuhudia. Ni mechi iliyokua na ushindani mkubwa sana. Iliisha kwa Barcelona kupata ushindi wa goli 4-3. Ilizalisha penati tatu, na kadi nyekundu moja.

Oktoba 28 itakua ni El Classico ya kwanza bila Cristiano Ronaldo tangu mwaka 2009. Lionel Messi hatokuwepo pia kutokana na majeraha. Kwa miaka tisa iliyopita mara nyingi kila ilipokua inakuja mechi hii, ni watu wawili waliokua wanazungumzwa.

Alizungumzwa Cristiano Ronaldo kwa upande wa Real Madrid na Lionel Messi upande wa Barcelona. Hawa ni wafalme wa soka ulimwenguni. Ni wachezaji wenye ushindani mkubwa.

Kwa kiasi kikubwa mechi hii iliamuliwa na mmoja wao. Ni Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ndio walioleta ushindani mkubwa na kuifanya mechi hii iwe kubwa zaidi.

Kwa sasa Cristiano Ronaldo hayupo tena Real Madrid. Lionel Messi ndiye nahodha wa Barcelona. Mambo yamebadilika. Barcelona na Real Madrid si timu zinazofuatiliwa na kuangaliwa sana kwa sasa.

Kuondoka kwa Cristiano Ronaldo kwa kiasi kikubwa kumeathiri sana kufuatiliwa kwa klabu hizi mbili, hata ligi ya soka nchini Hispania haina mvuto ule uliokuwepo kabla ya Cristiano Ronaldo kuondoka.

Itakua ni El Classico inayozihusisha klabu zenye matatizo mawili tofauti. Nimeiangalia Real Madrid msimu huu, nikaingalia Barcelona pia. Kabla ya hapo niliifuatilia vizuri timu ya taifa ya Hispania kwenye mashindano ya kombe la dunia June mwaka huu pale Russia.

Hispania ni timu inayoundwa na wachezaji wa Barcelona na Real Madrid kwa kiasi kikubwa. Hispania iliondolewa kwenye hatua ya mtoano. Ikishinda mechi moja na kutoa sare mechi tatu. Ilifunga magoli saba na kufungwa magoli sita.

Haikuwa kwenye kiwango bora. Matokeo waliyayapata yalikua nje ya matarajio. Matokeo yaliyosababishwa na wachezaji wenyewe. Wachezaji ambao wanatoka kwenye klabu za Real Madrid na Barcelona.

Real Madrid ya msimu ulipita ilifanikiwa kushinda ubingwa wa ulaya kwa msimu wa tatu mfululizo. Kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo yalibebebwa na Cristiano Ronaldo. Magoli yake yalikua na mchango mkubwa sana.

Alifunga nusu ya magoli yaliyofungwa na Real Madrid kwenye mashindano. Wahakufanya vizuri sana kwenye ligi, walimaliza wakiwa nafasi ya tatu. Licha ya hayo, bado mchango wa Cristiano Ronaldo ulionekana. Alihusika kwenye robo ya magoli yote ambayo Real Madrid iliyapata.

Si msimu huo tu, magoli ya Cristiano Ronaldo yamekua na maana kubwa sana kwa kipindi cha miaka tisa iliyopita. Leo hii Cristiano Ronaldo hayupo. Hayupo pia mchezaji mwingine mahiri mwenye uwezo wa kufunga magoli mengi.

Baada ya kundoka, Perez hakufanya usajili wa mshambuliaji mwingine anayeweza kumpa angalau magoli 30 ya msimu. Aliamua kumrudisha bwanamdogo Mariano Diaz ambaye alishawahi kufeli akiwa na Santiago Bernabeu. Hapo ndipo tatizo lilipo. Haishangazi kuona Real Madrid ikishindwa kupata goli kwa mechi tatu mfululizo.

Sergio Ramos, Marcelo, Daniel Carvajal na Raphael Varane ni miongoni mwa mabeki bora sana duniani. Kuna keylor Navas na Thibaut Courtois ambao ni magolikipa wazuri. Licha ya uwepo wao bado haizuii Real Madrid isifungwe magoli.

Na imekua hivyo kwa miaka mingi. Makosa yao ya kuruhusu magoli kufungwa yalifunikwa na magoli ya Cristiano Ronaldo. Ilikua ni rahisi kwa wao kuruhusu goli lakini Cristiano Ronaldo alifunga magoli mengi kule mbele ikawa rahisi kushinda mechi nyingi.

Kwa sasa wanakosa mkombozi anayeweza kufunga kule mbele. Kareem Benzema ameendelea kuwa yuleyule, mchezaji anayepoteza nafasi nyingi. Gareth Bale haeleweki. Marco Asensio amefunga goli moja tu.

Barcelona wao si imara tena kwenye eneo la ulinzi. Wamefungwa goli kwenye mechi saba kati ya tisa walichozesha msimu huu. Hiki ni kitu ambacho kinawaathiri sana.

Gerald Pique na Jordi Alba si wale tuliozoea kuwaona. Safu yao ya ulinzi inabebwa na Samuel Umtiti ambaye wakati mwingine hufanya makosa akijaribu kufuta uzembe wa kina Pique. Umtiti Hatokuwepo kwenye mechi hii.

Umahiri wa Sergio Busquet kwenye eneo la kiungo mlinzi umepungua pia. Ni Barcelona tofauti. Barcelona iliyo bora kwenye eneo la ushambuliaji pekee.

Wanaruhusu magoli mengi ya kufungwa. Kina Lionel Messi wanaposhindwa kufunga magoli mambo yanakua magumu. Jaribu kujiuliza itakua vipi Lionel Messi akikosekana kwenye mechi hii kama ilivyotajwa.

Naisubiri sana Oktoba 28. Nasubiri kuiona El Classico tofauti. El Classico inayozikutanisha Barcelona na Real Madrid zenye matatizo tofauti. El classico bila Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Zimebaki siku sita tu.

0754 896963