DC Katambi atangaza neema kwa Bodaboda, Apanga kuwapa Bima, Mikopo


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi amepanga kukutana na waendesha bodaboda na bajaji wote wa Jiji la Dodoma ili kusikiliza na kutatua kero mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili.

DC Katambi amewataka waendesha bodaboda wote na bajaji kufika katika mkutano huo siku ya Ijumaa ya Oktoba 19 kuanzia saa nane katika uwanja wa Jamhuri ambapo amepanga kuongozana na Kamanda wa kikosi cha barabarani wa wilaya hiyo, maafisa wa Kupambana na Kuzuia Rushwa TAKUKURU, Afisa maendeleo ya jamii kutoka jiji, SUMATRA na mashirika ya Bima.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema lengo kuu la mkutano huo ni kutoa elimu kuhusu ulinzi na usalama wao, kusajiliwa, kupata bima za afya, namna bora ya kutumia barabara, msamaha kwa makosa madogo, kuwa na umoja na nidhamu kwa jamii na Serikali huku pia wakipata fursa za mikopo.


" Niwasihi sana madereva wa bodaboda na bajaji ambao kimsingi wengi wenu ni vijana wenzangu kujitokeza kwa wingi, siku hiyo nitahitaji kama kijana mwenzenu na kiongozi wenu kusikiliza kero, changamoto na matatizo ambayo yanawakabili, ni jukumu langu kama msaidizi wa Rais Dk John Magufuli ambaye nyie mlimchagua kwa kura nyingi kukutana na nyie na kutatua changamoto zilizopo.

" Niwaombe mpeane taarifa ili asiwepo ambaye ataukosa mkutano huo, kutakua na mambo mengi ya kuzungumza na kupeana fursa  kama vijana, na Mbunge wetu wa Dodoma ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Anthony Mavunde atakuepo kutoa misaada mbalimbali," amesema DC Katambi.