WINGA WA MABINGWA WA SOKA TANZANIA BARA, SIMBA, SHIZA KICHUYA PICHA NA MTANDAO
Kichuya ambaye alitua Simba akitokea Mtibwa Sugar amekuwa akikosolewa na mashabiki wa timu hiyo kutokana na kushindwa kufunga mabao kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Winga huyo ambaye pia aliachwa katika kikosi cha timu ya Taifa kwenye michezo miwili dhidi ya Cape Verde, amesema wanaomkosoa wanatakiwa kuelewa katika kila mchezo kocha anampa "kazi maalumu" ya kufanya ili kusaidia ushindi na huwa anahitimiza.
“Bado naamini kiwango changu kipo juu, na bado nitaendelea kujituma mazoezini na kwenye mechi kuendelea kuwa juu, sifungi kila mechi kwa sababu ya majukumu ninayopewa na kocha wangu,” alisema Kichuya.
Aliongeza kuwa, kikubwa yeye anachozingatia ni kuona timu inapata ushindi katika kila mchezo ili waweze kufikia malengo ya pamoja.
“Nikipata nafasi ya kufunga nitafunga tu, mashabiki wasiwe na hofu, lakini kama ni nafasi ya kumtengenezea mchezaji mwenzangu kufunga bado nitafanya hivyo, cha msingi timu ipate ushindi,” aliongeza.
Kichuya amefunga bao moja katika michezo saba aliyoichezea Simba msimu huu akiwa na kikosi hicho kilichoko chini ya Mbelgiji, Patrick Aussems.
