WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI, LUHAGA MPINA PICHA NA MTANDAO
Agizo hilo alilitoa jana kutokana na kuwapo taarifa ya kushushwa kwa bei ya samaki katika viwanda vyote na kusababisha malalamiko kutoka kwa wavuvi, hivyo kuilazimu serikali kuingilia kati.
Akizungumza na wamiliki wa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki, wawakilishi wa vyama vya wavuvi, wavuvi, mawakala na wafanyabiashara wa samaki jijini Mwanza, Waziri Mpina alisema wamiliki hao wanapaswa kurejesha bei ya zamani na wasipofanya hivyo, serikali itaamua vinginevyo.
"Nataka kuweka msimamo kwamba serikali haikubaliani na uamuzi wa kushusha bei kwa hiyo wenye viwanda mnayo nafasi kabla serikali haijawapangia kwa sababu kama tutashindana, sisi tutaweka msitari kwamba samaki wa Tanzania watauzwa kwa bei hii," alisema Mpina
Mpina alisema wenye viwanda wanayo nafasi ya kufanya uamuzi sahihi wa kurejesha bei ya zamani na kusisitiza kuwa mawazo yanayotolewa kwamba wavuvi waruhusiwe kuuza samaki Kenya na Uganda, yanakwenda kinyume cha sera ya serikali inayohimiza viwanda.
"Bahati nzuri hatuwezi kukimbilia tu lile mnalosema la kuuza kwenye viwanda vya majirani. Tukifanya hilo tutaliwa, nenda kwa Omega pale ukaone vijana walioajiriwa pale nenda kwa TFP, nenda Musoma tukijichanganya kwamba tunaweza tukauza Kenya au wapi si sahihi,"alisema Mpina.
Alisema ikiwa wenye viwanda hawatatoa bei nzuri, serikali italazimika kutengeneza viwanda vingine vya wazalendo watakaotoa bei nzuri na zenye uwazi kwa wavuvi ili rasilimali hizo ziweze kulinufaisha taifa.
Akizungumza na wavuvi katika soko la kimataifa la samaki la Kirumba jijini Mwanza, Mpina alisifu uongozi wa Manispaa ya Ilemela kwa kazi nzuri ya kulisimamia soko hilo na kuwezesha kukusanya Sh. milioni 600 kwa mwaka na hutumia Sh. milioni sita tu kila mwezi kwa shughuli za soko sambamba na kutenga Sh. milioni 300 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu.
Pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Uvuvi, Dk. Rashid Tamatama, kuhakikisha vibali vya kusafirisha samaki nje ya nchi vinatolewa sokoni hapo tofauti na ilivyo sasa kwa wafanyabiashara kwenda hadi Ofisi za Uvuvi Nyegezi, hivyo kusababisha usumbufu kwa wahusika.
Pia alisisitiza kuwa ni dhamira ya serikali kuendelea kusimamia rasilimali za uvuvi ili kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho na kurejea kauli yake kwamba rasilimali hizo zinapaswa kutunzwa kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote na si kikundi cha watu wachache.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magesse Bulayi, alisema usimamizi wa rasilimali za uvuvi unafanyika kwa mujibu wa sheria zilizopo na kwamba watendaji wakuu wa wizara wataendelea kusimamia sheria hizo pamoja na maelekezo ya Waziri Mpina ili kuhakikisha sekta ya uvuvi inatoa mchango unaostahili kwa maendeleo ya taifa.
