Mkoa wa Dar es Salaam umetajwa kuwa ndio mkoa ulioongoza kwa kuzalisha taka miongoni mwa mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Nipe Fagio walioratibu tukio la Siku ya Usafi Duniani nchini, Ana Rocha, alisema kuwa zaidi ya watu 26,000 walishiriki tukio hilo ambapo zaidi ya tani 400 za taka zilikusanywa maeneo mbalimbali nchini.
Alisema miongoni mwa taka hizo sehemu kubwa zilikuwa taka za plastiki zinazotokana na vifungashio vya chakula na vinywaji, Alisema Dar es Salaam ndio mkoa ambao umeathirika zaidi na uchafu nchini.
“Dar es Salaam imeongoza kwa kuathirika zaidi na taka, taka nyingi tulizokusanya Siku ya Usafi Duniani zilitoka maeneo ya Buza Wilaya ya Temeke, eneo la Jangwani Wilaya ya Ilala pamoja na Kimara Mwisho Manispaa ya Ubungo,” alisema Rocha.
“Pamoja na kwamba tatizo la taka bado ni kubwa, uelewa wa jamii kuhusu madhara ya uchafuzi wa mazingira unaoongezeka na Watanzania wanajitokeza kuchukua hatua, tunawashukuru wote waliojitokeza pamoja na wadau waliosaidia kulifanya tukio hili liwe na mafanikio makubwa,”aliongezea Rocha.
Alisema Siku ya Usafi Duniani ambayo iliadhimishwa Septemba 15, Tanzania kulikuwa na matukio 102 ya usafi yalifanyika katika mikoa 13 na zaidi ya miji 30 ambapo jumla ya mifuko 18,547 ya taka ilikusanywa.
“Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba matukio ya kufanya usafi sio suluhisho la kudumu na hayawezi kuwa mbadala wa mifumo ya udhibiti taka.
Lengo la tukio hili ilikuwa ni kuhamasisha jamii kuhusu uchafuzi wa mazingira, kutoona taka na udhibiti hafifu wa taka.
Tukio hili lazima lifuatiwe na mageuzi katika udhibiti wa taka yakiongozwa na wenye viwanda nchini hususani ambao vifungashio vya bidhaa zao vinachangia tatizo la taka.
“Nawaasa wenye viwanda wote nchini kuchangia na kushiriki katika jitihada za kuweka mifumo ya ukusanyaji na udhibiti wa taka.
Plastiki na vifungashio vingine hazitakiwi kuchafua mito, kingo za barabara pamoja na bahari.
Taka ni rasilimali muhimu zinatakiwa kusagwa na kutumika kutengeneza bidhaa, hii itasaidia kuongeza ajira na kuboresha uchumi,” alisema Rocha.
Ukaguzi wa taka uliofanyika kwenye Siku ya Usafi Duniani ulibaini vyanzo vikuu vya uchafuzi wa mazingira ambapo taka nyingi zaidi zilibainika kuzalishwa na bidhaa maarufu nchini ikiwa ni pamoja na mifuko ya kubebea vitu, makopo na chupa za bia, vifungashio vya maziwa, chupa za maji, vifungashio vya sabuni, viberiti, ndala, pombe kali, vichungi vya sigara, ice cream na vinywaji baridi kama soda na juisi.
