Safari ya Cameroon? Inawezekana


Na Tom Thomas 

Ghafla nimekumbuka kitu. Taifa Stars ilicheza na Lesotho June 10 mwaka jana pale Azam Complex. Mechi ikamalizika kwa sare. Alianza Mbwana Samata kufunga kwa mpira wa adhabu ndogo kabla ya Thapelo Thale kusawazisha.

Baada ya mechi kocha wa Lesotho hakuamini kama amepata sare. Aliwapongeza wachezaji wake angalau kwa kuondoka na alama moja. Hakuamini kama Taifa Stars yenye Mbwana Samata, mchezaji aliyemuogopa zaidi imeshindwa kupata ushindi tena kwenye ardhi yake ya nyumbani.

Nimeikumbuka mechi hii. Kama tungepata ushindi ina maana tungekua na alama saba sasa. Nyuma ya Uganda wenye alama kumi. Achana na mechi zingine, mechi hii iliyopita dhidi ya Lesotho tulihitaji sana ushindi.

Bahati mbaya haikua hivyo. Hata hivyo huu si muda wa kukumbuka yaliyopita. Ni muda wa kutafakari yanayofuatia. Bado tuna nafasi nzuri ya kwenda Cameroon.

Timu mbili zitafuzu. Ni wazi Uganda wana uhakika tayari. Kazi ni kwetu. Cape Verde na Lesotho wana nafasi, sisi tuna nafasi pia. Tumebakiwa na mechi mbili muhimu, mechi ambazo zinaweza kuandika historia.

Kwa miaka mingi tumekua wasindikizaji tu kwenye safari za Afcon au kombe la dunia.Safari hii inawezekana. Ni muda wa kuungana na kushirikiana kwa pamoja.

Tutakwenda Lesotho kutafuta pointi tatu tu. Hatuhitaji matokeo mengine zaidi ya ushindi. Kitu kizuri ni kwamba, wao wanatuheshimu. Bado wana kumbukumbu ya kilichotokea kwenye mashindano ya Cosafa.

Baada ya hapo tutarudi nyumbani, kucheza na Waganda mechi ya mwisho. Tutahitaji pointi tatu pia kutoka kwao. Ndio, inawezekana. Tutakua kwenye ardhi yetu ya nyumbani.

Kwa umoja wetu tunaujaza uwanja na kuwapa sapoti kubwa wachezaji wetu kama vile Wakenya walivyofanya mechi iliyopita. Hakika inawezekana.

Lesotho na Cape Verde wao wasipopata pointi sita hawatokwenda Cameroon. Sisi tuna faida. Kama tutapata angalau pointi nne huku Uganda akiwafunga Cape Verde tunakwenda Cameroon.

Haya yote yanawezakana kama tutaamua kukaa chini kwa pamoja tukiziondoa tofauti zetu za Simba na Yanga huku tukiendelea kumsapoti kocha wetu Emmanuel Amunike.

Licha ya kuwepo kwa matatizo mengi yanayokwamisha mafanikio ya Taifa Stars, hili la Usimba na Uyanga ni tatizo kubwa. Hasa kwa mashabiki wengi nchini.

Watanzania wengi wanazipenda Simba na Yanga kuliko timu ya taifa. Wanapenda wachezaji wao zaidi kuliko wachezaji wa timu nyingine.

Ndio maana licha ya Taifa Stars kufanya vizuri mechi iliyopita, bado mashabiki wa Simba walihitaji kumuona kiungo wao Jonas Mkude akiwa uwanjani huku wale wa Yanga wakimuhitaji Ibrahim Ajibu.

Hawakujali kuhusu matokeo yaliyopatikana. Yanga walisifia uwezo wa Kelvin Yondani, Simba wakamsifia Erasto Nyoni. Ndivyo mpira wetu ulivyo.

Kuna wakati mchezaji wa Yanga akifanya vibaya mashabiki wa Simba watafurahi, mashabiki wa Yanga pia hufurahi kuona mchezaji wa Simba akifanya vibaya timu ya taifa.

Kuna wale wengine ambao huondoa mapenzi yao kwa timu ya taifa baada ya kuona mchezaji wao wanayempenda hayupo kwenye kikosi, au pengine hajapangwa kwenye kikosi cha kwanza. Wako radhi washabikie timu pinzani.


Sasa ni muda wa kuacha haya yote. Tuungane kwa pamoja angalau kwa mechi hizi mbili tupate matokeo twende Cameroon. Sisi ni taifa moja.

Tunatamani kuwaona wachezaji wetu kama vile tulivyozoea kuwaona wachezaji wa Nigeria, Ivory Coast na Senegal. Kama Uganda walionekana mashindano yaliyopita sisi ni kina nani hadi tushindwe?

Tuna kikosi kizuri, tuna wachezaji wengi wazuri. Tuna magolikipa wazuri, tuna mabeki mahiri walio bora kwa sasa. Tuna viungo wazuri wengi. Washambuliaji wanaofanya vizuri wapo pia. Hata anapokosekana mmoja, kuna mmoja anayeweza kuziba nafasi vizuri.

Tuna kila sababu ya kwenda Cameroon. Kitu kizuri ni kwamba hata serikali imekua msitari wa mbele kuhakikisha Taifa Stars inafanya vizuri. Ni swala la kuendelea kuisapoti tu timu yetu kwa pamoja. Inawezekana.

Safari ya Cameroon inaweza fungua milango mingi kwa wachezaji wetu kwenda mbele zaidi. Tunatamani kuwaona kina Mbwana Samata wengi barani Ulaya. Hii yote itawezekana kama tutaungana na kushirikiana kwa pamoja. Taifa Stars ni yetu sote.

0754 896963