Simu za Viongozi zamiminika kwa Ney, wapagawa na ngoma yake mpya


MKALI kutoka kisiwa cha Bongo Fleva Ney wa Mitego amefichua kuwa amekuwa akipokea ujumbe na simu nyingi za kumpongeza kutokana kwa viongozi mbalimbali nchini baada ya kuachia kibao chake cha Alisema.

Ney ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu ameachia ngoma mpya Oktoba 6, mwaka huu ambayo imebeba maudhui yanayolenga maisha ya wananchi wengi, viongozi wa Serikali na upinzani na wandishi wa habari huku pia akikumbushia mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwilin aliyeuwawa kwa risasi Februari 16 mwaka huu kwenye maandamano ya Chadema, Kinondoni.

Amesema wengi ambao wamekuwa wakimpigia wanamueleza kuwa wamefurahishwa na mashairi ya ngoma hiyo na namna alivyotumia kionjo cha wimbo wa zamani uliokuwa ukitumika mashuleni ukimzungumzia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

" Napokea simu na msg nyingi za pongezi kutoka kwa viongozi tofauti tofauti wengine sijawai kuwaza hata kuzungumza nao au kuhisi kama wanasikilizaga hata nyimbo zangu. Watu wa kawaida pia kuhusu huu wimbo  ‘Alisema’ najiuliza nini kikubwa kipo kwenye hii ngoma?

Maneno niliyoongea? Beat? Style niliyoimba? Chorus? kama ni verse ipi ya kwanza ya Pili? Au watu wamechoshwa na nyimbo za mapenzi kila siku.? Huu ni wimbo wa Taifa🇹🇿”Ameandika Nay wa Mitego